Baada
ya kusota rumande kwa takribani siku saba, hatimaeMwenyekiti wa klabu
ya Yanga, Yusufu Manji amepandishwa katika kizimba cha Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma za matumizi ya dawa za kulevya.

Manji
ambae pia ni Diwani wa Mbagala Kuu na mfanyabiashara maarufu
ameshtakiwa chini ya kifungu cha sheria namba 17(1)(a) ya sheria ya
kuzuia na kupambana na dawa za kulevya namba 5 ya mwaka 2015. 



Amesomewa mashtaka yake leo na karani wa mahakama hiyo, Sarah Mulokozi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkeha.

Manji
amekananusha kutumia dawa za kulevya na yuko nje kwa dhamana baada ya
kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kuweka dhamana ya milioni kumi
na mdhamini mmoja ambaye nae ameweka kiasi hicho hicho cha dhamana

Manji
alifika mahakamani hapo saa nane kasoro nne na alipandishwa mahakamani
majira ya saa tisa. Katibu wa klabu hiyo, Charles Boniphace Mkwasa
ndiye aliyemuwekea dhamana Manji na kumfanya awe huru.

Katika
kesi hiyo Manji anatetewa na mawakili watatu waliokuwa wakiongozwa na
wakili Alex Mgongolwa, Hudson Ndusyepo na Jeremiah Mtobesya huku upande
wa Jamuhuri ukiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa mashtaka, Oswald
Tibabyekomya aliyekuwa akisaidiana na wakili wa serikali Shadrack
Kimaro.

Akisoma hati ya mashtaka, Mulokozi amesema kuwa, kati ya
Februari 6 na 9 mwaka huu huko Upanga Sea View ndani ya Wilaya ya
Ilala jijiini hapa, mshtakiwa alitumia dawa za kulevya aina ya Heroine
(diacefyl Morphine)..

Mara baada ya kutimiza masharti ya dhamana
Manji aliondoka katika viwanja vya mahakama hiyo akiwa katika gari aina
ya Hummer lenye namba za usajili T 670 BBX huku akisindikizwa na umati
wa mashabiki wa Yanga.