Mabingwa watetezi wa Kombe la FA Manchester United wamefungwa goli 1-0 na Chelsea katika nusu fainali iliyochezwa Stamford Bridge.
Bao pekee la ushindi kwa Chelsea lilifungwa na N'Golo Kante kwa mkwaju mkali katika dakika ya 51. Manchester United walicheza kwa kipindi kirefu wakiwa mchezaji mmoja pungufu baada ya Ander Herera kuoneshwa kadi mbili za manjano katika dakika ya 35.
Kadi nyekundu
Mchezo ulibadilika baada ya Ander Herera kutolewa kwa kumchezea rafu Eden Hazard. Kipa wa United, David De Gea awali aliokoa mkwaju mkali wa Hazard.
Kikosi cha Antonio Konte kilitumia mwanya wa kutolewa kwa Herera katika kipindi cha pili na Kante kufunga bao zuri kwa shuti la mbali.
Mchezo huo ulighubikwa na hasira, huku Diego Costa na Marcos Rojo wakizozana mara kwa mara, wakati meneja Antonio Conte naye akikwaruzana na Jose Mourinho.
Marcus Rashford, ambaye wengi hawakutarajia angeweza kucheza kwa kuwa alikuwa mgonjwa, alipata nafasi nzuri ya kusawazisha goli, lakini kipa wa Chelsea Thibault Courtois alizuia mkwaju wake.
Chelsea hawakuweza kuongeza goli licha ya kupata nafasi kadhaa, lakini ni safari nyingine kwa Mourinho kusahau kwa kuwa anafungwa mara ya pili katika klabu yake ya zamani, baada ya kutandikwa 4-0 kaika mchezo wa Ligi Kuu mwezi Oktoba.
Chelsea watakutana na Tottenham katika mchezo wa nusu fainali utakaochezwa tarehe 22 mwezi Aprili kwenye uwanja wa Wembley. Nusu fainali nyingine ni kati ya Arsenal watakaocheza na Manchester City Aprili 23.
0 Comments