Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amepiga marufuku uchimbaji wa kokoto katika eneo la Boko Chama na ametoa siku saba kwa wachimbaji kuondoa kokoto zilizopo eneo hilo.
Amesema amechukua hatua hiyo kutokana na hali ya hewa kipindi hiki cha mvua na kusisitiza kuwa ikiwa machimbo hayo hayatafungwa, yanaweza kuleta athari kwa jamii.

Ametoa amri hiyo jana akiwa kwenye ziara yake ya siku 10 kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi na kutatua kero za wananchi.
"Muache hii kazi ya kuchimba kokoto hapa, hiki ni kipindi cha mvua kwa hiyo athari zingine tunaweza kuzizuia sisi wenyewe, acheni kuchimba ili watu wawe salama," alisema Hapi.
Ameagiza Ofisi ya Mazingira na Mipango Miji kuliangalia eneo hilo na kulibadilisha kuwa dampo la taka kwa ajili ya eneo hilo.
Amesema wanapochimba kokoto hasa katika kipindi hiki cha mvua kunasababisha mmomonyoko wa ardhi ambao ni hatari kwa usalama wa makazi ya watu.
Katika hatua nyingine, aliagiza Idara ya Mipango Miji katika wilaya hiyo kuhakikisha wananunua ramani na kuzisambaza kwa watendaji kata ili waweze kufahamu mipaka na maeneo yao ya wazi.
Amesema uuzwaji na uvamizi wa maeneo ya wazi umekithiri na kwamba baadhi ya viongozi wasio waaminifu wamekuwa wakijihusisha na kuuza maeneo hayo.