Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki
WAKUU wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kusini mwa Afrika wametakiwa kuongeza ushirikiano katika kubadilishana taarifa za wahalifu na uhalifu unaovuka mipaka ili kuufanya Ukanda wa Kusini mwa Afrika kuwa salama.
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki alisema hayo mjini Bagamoyo mkoani Pwani alipofungua mkutano wa siku mbili wa Wakuu wa Upelelezi wa Polisi kutoka Shirikisho la Wakuu wa Polisi kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO) unaofanyika sanjari na Kamati za Ufundi za SARPCCO ili kupanga mikakati ya kupambana na uhalifu na wahalifu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, Kaniki alisema ili kuwabaini wahalifu kwa urahisi, ni vema ushirikiano wa kubadilishana taarifa ukafanyika kwa haraka hasa kwa kuimarisha teknolojia ya habari na mawasiliano; na mafunzo kwa maofisa wa polisi ili kuwajengea uwezo wa kubaini mapema viashiria vya uhalifu katika maeneo yao.
Aliziomba serikali za nchi wanachama kuendelea kutenga bajeti zinazokidhi mahitaji ya majeshi ya polisi ili kuyawezesha kufanya kazi kwa ufanisi.
Kaniki amesema majeshi hayo hayana budi kuzingatia nidhamu ya matumizi ya fedha zinazotengwa ili kuimarisha mifumo ya kuzuia na kupambana na uhalifu.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, DCI Robert Boaz alisema umoja huo utaendelea kuandaa operesheni za pamoja katika kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka unaohusisha wizi wa magari, dawa za kulevya, biashara haramu ya usafirsishaji wa binadamu, uharamia na ujangili.
Boaz alisema mkutano huo utajadili kwa kina utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika mkutano wa wakuu wa polisi uliofanyika mwezi Septemba mkoani Arusha na kuweka mikakati endelevu ya kukabiliana na uhalifu.
Mkuu wa Shirikisho la Polisi wa Kimataifa (INTERPOL) Kanda ya Kusini, Mubita Nawa alisema umoja huo umepata mafanikio makubwa kutokana na operesheni mbalimbali zinazofanyika mara kwa mara katika kukabili uhalifu, huku akibainisha kuwa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu bado ni changamoto kwa nchi wanachama.
Shirikisho la Wakuu wa Polisi Kusini mwa Afrika (SARPCCO) lipo chini ya Uenyekiti wa Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania.
Hivi sasa umoja huo unaundwa na nchi 15 ambazo ni Tanzania, Angola, Botswana, Malawi, Lesotho, Mauritius, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Swaziland, Madagascar na Shelisheli.