WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira na Muungano, January Makamba ameagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kaskazini kufanya tathmini ya mazingira katika Hoteli ya Ngaresero Lodge.

Aidha, mmiliki wa hoteli hiyo amepewa siku 10 kufanyiwa tathimini ya mazingira ili kudhibiti matumizi ya maji kwa mwekezaji huyo pamoja na vijiji vinavyozunguka eneo hilo.
Makamba alitoa agizo hilo jijini hapa alipokuwa kwenye ziara ya kujionea hali halisi ya mazingira pamoja na athari zake katika mikoa mbalimbali.
Alisema mmiliki wa hoteli hiyo ana kibali cha mazingira cha awali na hivi sasa sheria hiyo imebadilishwa hivyo anapaswa kujua kuwa sheria zimebadilika na anapaswa kutumia watu sahihi wanaojua mazingira na kufanyiwa tathimini ya mara kwa mara.
“Tumeona uwekezaji ulioufanya lakini hapa kuna dosari kwa nini hujafanyiwa tathimini ya kimazingira, lakini pia ni lazima ujue kibali kinatolewa kama umekidhi viwango vya utunzaji wa mazingira pia haya maji ugawe vijijini muandae utaratibu wa mgawo wa maji na si kuyadhibiti kwako tu,” alisema.
Mmoja kati ya wamiliki wa hoteli hiyo, Tim Litch alikiri kuwapo uzembe katika tathimini ya kimazingira katika eneo hilo na kuomba mamlaka husika kushirikiana naye ili kurekebisha kasoro hizo kwani eneo hilo analitumia kwa ajili ya utalii, kufuga samaki pamoja na kuhakikisha mazingira yakuwa safi.