WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye amesema yeyote mwenye ushahidi kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na Wema, aweke ushahidi wake wazi na yupo tayari kuwajibika kwa hilo.
Nape ameyasema hayo katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na Televisheni ya ITV kila Jumatatu, ambako mbali na kuzungumzia suala hilo, pia alisimamia kauli yake ya kuchafuliwa kwa ‘brand’ za watu katika kupiga vita dawa ya kulevya.
Alizungumzia suala hilo wakati alipoulizwa kuhusu kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambayo alikaririwa akisema, “kuna watu wanapiga kelele kwa vile nimewagusa wapenzi wao, kama mtu unampenda msaidie atoke kwenye matumizi ya dawa za kulevya.”
Lakini Nape akizungumzia suala hilo, alisema “Sina uhusiano wowote wa kimapenzi na Wema, yeyote mwenye ushahidi aweke wazi nipo tayari kujiuzulu.”
Nape amesema ataendelea kusimamia msimamo wake kuwa nia ya kupambana na dawa za kulevya ni njema, ila njia iliyokuwa inatumika ilikuwa si sahihi.
“Ukinitaja jina ukaniambia baada ya siku mbili njoo kituoni hata kama nilikuwa na dawa za kulevya nyumbani kwangu utayakutaje, nitayaficha nitakuja kuripopti kituoni,” amesema Nape na kuongeza:
“Utanibana nitakwambia twende nyumbani kwangu ukakague, utakagua hutoyakuta, nia ilikuwa njema, lakini utaratibu ulikuwa mbovu, huwezi kushughulika na watumiaji ukadhani ni wahalifu wako, unakosea kwa sababu hapa kuna watumiaji na wauzaji na wale wanaoleta.
“Ukishughulika na mtumiaji huyu ukadhani ndiye mhalifu wako unakosea, kwa sababu huyu ni muathirika na muathirika anahitaji dawa anahitaji huduma ameshaathirika, hapa wahalifu wetu ni kuanzia huyu anayemletea halafu kuna huyu anayempa yule aliyemletea, sasa ili uwapate hawa wawili lazima umtumie huyu vizuri ili akupeleke kwa hawa wawili…..Lakini ukimkamata huyu ukamtia ndani sasa hawa wawili watakimbia.”
Aliongeza, “Kwa hiyo mimi nikaona tunaivuruga vita yenyewe, anayeingiza dawa za kulevya na anayesambaza kwa maana ya kuyauza, hawa ndiyo tatizo letu.
“Na ndio maana nikasema hebu tutumieni busara, watu wakadhani nimepinga, tena mimi nilisema mara nyingi sana tumieni busara namna ya kuiendesha vita hii.
“Madhara ya kutotumia busara katika vita hii ni makubwa sana, kwa sababu ukimweka huyu mtu mmoja ndani hawa wengine wataendelea kuwaathiri wengine na ndiyo maana nasema hii vita tutumieni busara.
“Hii vita ni ya kupigana kimya kimya kwa sababu wanaofanya biashara hii hawaifanyi hadharani wanafanya kwa kificho, shughulika nao kwa kificho, hii vita hakuna mahali ambapo wameshawahi pigana hadharani, tukitajana hadharani hata wenye chuki watatajana humo humo,” amesisitiza.
|
0 Comments