Sehemu ya hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar

WAGONJWA zaidi ya 600 wamepatiwa matibabu ya upasuaji wa uti wa mgongo na vichwa maji kupitia kitengo cha upasuaji wa maradhi hayo ambacho kinatimiza miaka miwili tangu kuanzishwa kwake.

Baada ya kuanzishwa kwa kitengo hicho na kuanza kutoa huduma, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh bilioni moja zilizotengwa kwa ajili ya kusafirishwa wagonjwa kwenda nje ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, Dk Jamala Adam Taib alisema hayo wakati alipokuwa anazungumzia mafanikio ya kitengo hicho tangu kilipoanzishwa.
Alisema matatizo ya vichwa maji kwa watoto awali lilikuwa moja ya tatizo kubwa lililoathiri maendeleo ya afya za watoto na kulazimisha wazazi kutumia fedha nyingi kupata huduma za matibabu kwa wagonjwa.
“Tangu kuanzishwa kwa kitengo cha kutibu matatizo ya vichwa vikubwa pamoja na uti wa mgongo tayari tumetibu jumla ya wagonjwa 600 ambao kabla ya hapo ilikuwa wasafirishwe na kupelekwa nje ya nchi,” alisema.
Alisema hayo ni mafanikio makubwa yaliyopatikana katika hospitali ya Mnazi Mmoja ambayo inakaribia kuwa hospitali ya rufaa.
Waziri wa Afya, Mahmoud Thabit Kombo alisema kuwepo kwa huduma mbalimbali za matibabu katika hospitali hiyo ikiwemo upasuaji kwa kiasi kikubwa kumeipunguzia mzigo Serikali kusafirisha wagonjwa kwenda nje ya nchi.
“Tumefanikiwa kuokoa kiasi kikubwa cha fedha serikalini ambazo zilikuwa zitumike kusafirisha wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu,” alisema.
Serikali ya Uholanzi imesaidia kwa kiasi kikubwa kujenga jengo la kisasa la kutoa huduma za upasuaji kwa wagonjwa wa maradhi mbalimbali yakiwemo ya uti wa mgongo, vichwa maji kwa watoto na figo.