Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Madaba, Shafi Mpenda
WATUMISHI wa umma katika halmashauri ya wilaya ya Madaba wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wametakiwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Aidha wale wanaoona hawawezi kuendana na kasi ya Dk John Magufuli ni vema wakajiondoa wenyewe kabla mkono wa serikali haujawafikia.

Kauli hiyo imetolewa na mkurugenzi wa halmashauri hiyo Shafi Mpenda.
Mkurugenzi huyo alisema kwamba watumishi wanaokwenda kwa mazoea hawahitaji kusubiri mpaka watakapoanza kuchukuliwa hatua kwani madhara yake kwa kawaida huwa makubwa.
“Awamu ya tano tumejipanga kuhakikisha kazi zote za maendeleo kwa wananchi zinatekelezwa kwa wakati ili kumaliza kero, serikali haitaki kuona mtumishi akifanya mambo ya ovyo na kuwa kituko kwa jamii inayomzunguka,” alisema Mpenda.
Mpenda amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kuwa waadilifu, waaminifu na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kukwamisha mipango mbalimbali ya serikali.
Mpenda alisema, halmashauri inataka kuona wananchi wa Madaba wanahudumiwa na kupata huduma stahiki kwa misingi ya sheria, haki na taratibu na haitakuwa na upendeleo katika kuwafikishia wananchi huduma bora za kijamii.