TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mara imewafikisha Mahakamani madaktari wawili wilayani Butiama kwa makosa ya kupokea rushwa kutoka kwa wagonjwa waliokuwa wanawahudumia.
Taarifa iliyotolewa na Takukuru Dar es Salaam iliwataja waliofikishwa mahakamani kuwa ni mmiliki na Mganga Msaidizi Mfawidhi Kliniki binafsi ya Basalia, Job Mwita Giryago na Mganga Msaidizi Mfawidhi Kituo cha Afya cha serikali Kiagata Marcelina Narkiso Magana.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani jana mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Msaloche wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mara na kusomewa mashtaka matatu ya rushwa na mwendesha mashtaka wa Takukuru William Fussi.
Katika shitaka la kwanza washtakiwa wamedaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Januari na Februari, mwaka huu walipokea rushwa ya Sh. 350,000 kutoka kwa mgonjwa Nyabwire Mwikabe ili afanyiwe upasuaji katika Kituo cha Afya Kiagata.
Katika shitaka la pili washtakiwa wamedaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Januari na Februari, mwaka huu walipokea rushwa ya Sh. 350,000 kutoka kwa mgonjwa Justine Matinde ili afanyiwe upasuaji katika Kituo cha Afya Kiagata.
Katika shitaka la tatu washtakiwa wamedaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Januari na Februari, mwaka huu walipokea rushwa ya Sh. 350,000 kutoka kwa mgonjwa Spora Juma ili afanyiwe upasuaji katika Kituo cha Afya Kiagata.
Mbali na mshitakiwa wa pili Marcelina Magana kukana mashitaka yote matatu mshtakiwa wa kwanza Job Giryago hakuwepo mahakamani wakati shauri dhidi yao lilipofunguliwa na kusomwa.
Upande wa Mashtaka uliiambia Mahakama kuwa uchunguzi wa shauri umekamilika na uliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutaja shauri kwa vile mshtakiwa wa kwanza hajafikishwa mahakamani.
Kesi imeahirishwa hadi Aprili 13, mwaka huu itakapotajwa tena na Magana yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh milioni 5, kila mmoja.