Waendesha mashtaka katika jimbo la Kaduna Kaskazini mwa Nigeria wamelimelishtaki kundi moja la watu 53 kwa kufanya njama za kutaka kusherehekea harusi ya watu wa jinsia moja.
Washukiwa waliokamatwa Jumamosi iliopita wamekana madai hayo huku mawakili wao wakisema kuwa walizuiliwa kimakosa.

Mahakama ililiwachilia kundi hilo kwa dhamana na kesi hiyo ikatajwa kuendelea manmo mwezi Mei.
Vitenndo vya wapenzi wa jinsia moja vimepigwa marufuku nchini Nigeria na hukumu yake ni miaka 14 jela.
Wakati walipowasilishwa mahakamani katika eneo la Chediya-Zaria, kundi hilo lilikana mashtaka hayo ya kupanga njama, kupanga mkutano haramu mbali na kujishirikisha na kundi haramu.
Wakili wa washukiwa hao Yunusa Umar alisema kuwa washukiwa hao ni wanafunzi na kwamba walikuwa wakizuiliwa kimakosa kwa zaidi ya saa 24, kulingana na gazeti la Premium Times nchini humo.
Wanaharakati wa maswala ya wapenzi wa jinsia moja ambao wamekuwa wakizungumza na washtakiwa hao wameambia ripota wa BBC Stephanie Hegarty mjini Lagos kwamba washukiwa hao walikamatwa katika sherehe za kuzaliwa na wala sio harusi.
Taifa la Nigeria lina idadi kubwa ya Wakristo kusini mwa taifa hilo na Waislamu katika eneo la kaskazini wote wakiwa wanapinga mapenzi ya jinsia moja.
Mnamo mwezi januari 2014, Polisi wa Kiislamu katika jimbo la bauchi walivamia maeneo kadhaa na kuwakamata makumi ya watu wanaoshukiwa kwa kutekeleza vitendo vya ulawiti.
Baadhi ya watu hao baadaye waliwasilishwa mbele ya mahakama ya sheria kwa dhamana huku umati wa watu waliojawa na ghadhabu ukikongamana nje.
Mahakama hiyo ilipigwa mawe na kesi hiyo ikasitishwa.Polisi walilazimika kufyatua risasi hewani ili kuutawanya umati huo na kuwarudisha washukiwa hao jela ijapokuwa hata ndani ya jela huenda wakashambuliwa.
Marufuku ya mapenzi ya jinsia moja ilioanza 2014 ,hutumiwa na maafisa wa polisi na wanachama kuhalalisha unyanyasaji dhidi ya wapenzi wa jinsia moja kulingana na shirika la Human Rights Watch.