ZAIDI ya watu 100,000 wana ugonjwa wa kifua kikuu (TB), lakini wapo majumbani jambo ambalo ni hatari kwa sababu wanatakiwa kupelekwa hospitalini kwa ajili ya kupata huduma, Bunge limeelezwa.
Hayo yamesemwa bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipokuwa akiongezea majibu yaliyotolewa na Naibu Waziri, Dk Khamis Kigwangalla.

Ummy amesema mgonjwa wa kifua kikuu akiachwa bila ya kupata huduma ana uwezo wa kuwaambukiza watu 20 kwa mwaka.
Amewaomba wabunge kuona umuhimu wa kuwahamasisha wananchi wao kuhusu ugonjwa huo wanapokuwa majimboni.
Vilevile, alisema ili kukabiliana na hali hiyo, serikali imeweka mpango kwa kila mjamzito na mtoto wa umri wa miaka chini ya mitano kupimwa Kifua Kikuu na Ukimwi ili kupata takwimu sahihi.
Katika swali hilo, Mbunge wa Busanda, Lolesia Bukwimba (CCM), ambaye alitaka kujua kama serikali inafahamu tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu limeathiri watu wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini na wale wanaoishi kandokando na maeneo ya wafugaji.
Pia, alihoji serikali ina mkakati gani wa makusudi wa kupambana na ugonjwa huo na silicosis hasa katika maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini.
Akijibu swali hilo, Dk Kigwangalla amesema Tanzania inafahamu uwepo wa magonjwa ya kifua kikuu na silicosis katika maeneo ya wachimbaji.
Naibu Waziri amesema kwa upande wa kifua kikuu inakadiriwa kuwa ukubwa wa tatizo hilo ni kubwa zaidi ikilinganishwa na hali halisi katika maeneo mengine.
Kuhusu silicosis, amesema kumekuwepo na ripoti za wagonjwa ambao ni wachimbaji wadogo wachache katika hospitali za serikali ikiwemo Kibong'oto.
Hata hivyo, alisema serikali kupitia halmashauri zilizo katika maeneo ya migodi imeanza kuweka mikakati ya kudhibiti magonjwa hayo kwa kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria.