KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Mfaume Kizigo amepongeza uongozi wa CCM Kibaigwa kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 kwa vitendo na kuzalisha ajira zaidi ya 800.
Alitoa kauli hiyo juzi wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali katika kata ya Kibaigwa, ikiwemo ujenzi wa chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya Kibaigwa, ukarabati wa soko la mboga na matunda katika kata hiyo lenye takribani vibanda 800. Kizigo ampongeza Diwani wa Kata hiyo na uongozi wa CCM wa kata chini wa Katibu Kedmon Chilongola kwa kusimamia na kuhangaikia matatizo ya wananchi kwa vitendo na kusisitiza umoja kwa wajumbe wa halmashauri kuu ya kata ya Kibaigwa.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 diwani wa Kibaigwa, Richard Kapinye alibainisha kuwa walifadhiliwa fedha kiasi cha Sh milioni 166.8 na Taasisi Local Investment Climate (LIC) kwa ajili ya ukarabati wa soko hilo. Alisema waliweza ukarabati banda la kuuzia samaki, mchele, nyanya na banda la matunda, ujenzi wa choo chenye matundu nane, vizimba viwili vya taka ngumu, ujenzi wa mabanda mawili mapya ya kuuzia mboga, kuingiza umeme, mifereji ya kuzuia maji kuingia katika soko hilo. Alisema maendeleo ya mradi huo kwa sasa ni asilimia 92 na unatarajiwa kuzinduliwa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Juni 2017.
Kizigo alishuhudia ujenzi wa chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya Kibaigwa unaogharimu Sh milioni 30 na sasa ujenzi upo hatua ya kutandika jamvi na Katibu wa Kamati ya Ujenzi ambaye ni daktari mkuu wa kituo hicho Shalua Mkumbo alisema baada ya wiki mbili ukuta wa jengo hilo utakuwa umekamilika. Kapinye alisema Kituo cha Afya Kibaigwa tayari kimepata mashine ya kupimia magonjwa (Ultrasound) na Kampuni ya Serengeti Brewerries Ltd imechimba kisima kirefu cha maji cha kutumia umeme wa jua chenye thamani ya Sh milioni 83 katika zahanati ya Kibaigwa. Pia katika kijiji cha Ndurugumi kilichimbwa kisima cha maji cha thamani ya Sh milioni 18 na ukarabati wa tangi kwa sasa eneo hilo wameondokana na shida ya maji iliyokuwa ikiwakabili 2016/1017 na hadi kufikia sasa katika kata hiyo kuna zaidi ya vichoteo 10 vya maji .
Aidha Kizigo alitembelea mradi wa choo uliokamilika katika shule ya msingi Miembeni chenye matundu 16 uliojengwa kwa ufadhili wa Ubalozi wa Afrika Kusini na kusisitiza kuwa serikali iliyopo madarakani ndio inaunganisha ufadhili huo. Kizigo amewasisitiza wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Kata hiyo kuhakikisha chama kinakuwa imara kwa kutunza siri za chama na kuhakikisha wanapofanya uchaguzi kuchagua viongozi kuanzia ngazi ya tawi wanaoelewa wapi Tanzania inapoelekea. Kwa upande wao wananchi wa kata hiyo wameipongeza serikali ya CCM kwa kuboresha huduma za kijamii kwa kasi hususani kituo cha afya na mazingira ya soko kwani wafanyabiashara wataongezaka.