Rais wa Marekani Donald Trump amesema karibuni wabunge wa vyama vya Democratic na Republican watamshukuru kwa kumfuta kazi mkuu wa FBI James Comey.
Akiandika kwenye Twitter, Bw Trump ametetea uamuzi wake ulioshangaza wengi wa kumfuta kazi mkuu huyo wa Shirika la Uchunguzi wa Jinai Marekani (FBI).
Rais huyo alimfuta kazi kutokana na jinsi alivyoshughulikia uchukuzi wa barua pepe za aliyekuwa mpinzani wa Bw Trump Hillary Clinton.
Bw Comey alikuwa anaongoza uchunguzi wa FBI kuhusu uhusiano kati ya maafisa wa kampeni wa Trump na Urusi.
Kufutwa kazi kwake kumewashangaza wengi Washington na maafisa wa chama cha Democratic pia wameeleza kushangazwa na uamuzi huo.
Kufutwa kwake "kumeibua maswali kuhusu iwapo ikulu ya White House inaingilia wazi uchunguzi wa jinai," alisema Adam Schiff, ambaye ni mwanachama wa ngazi ya juu zaidi kutoka chama cha Democratic katika kamati ya bunge kuhusu ujasusi.
Lakini kiongozi huyo ametetea uamuzi wake Jumatano asubuhi, saa chache kabla ya kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov - mkutano wa kwanza kati ya Trump na maafisa wa Urusi tangu achukue hatamu Januari.
"Nafasi ya James Comey itajazwa na mtu ambayea naweza kufanya kazi hiyo vizuri sana, na kurejesha moyo na fahari ya FBI," amesema Bw Trump.
"Comey alipoteza imani katika kila mtu Washington, miongoni mwa Wanarepublican na Wanademocrat. Mambo yakitulia, watakuwa wananishukuru!" aliongeza.
Hii ni mara ya pili pekee kwa mkuu wa FBI kufutwa kazi katika historia ya Marekani.
Msemaji wa ikulu ya Urusi Dmitry Peskov amesema kufutwa kazi kwa Bw Comey ni "suala la ndani" la Marekani na "halina uhusiano wowote na Urusi", kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya Urusi TASS.
Hayo yakijiri, kiongozi wa walio wachache bungeni Chuck Schumer amesema atawasilisha ombi kuwepo na kikao cha maseneta wote wapewe taarifa na maafisa wakuu wa wizara ya haki ya Marekani.
Aidha, ameomba kuwepo na mwendesha mashtaka maalum wa kuongoza uchunguzi wa FBI kuhusu uwezekano wa uhusiano kati ya maafisa wa Urusi na maafisa wa kampeni wa Bw Trump.
Mbona James Comey akafutwa?
Bw Trump aliandika kwenye barua kwa Bw Comey kwamba aliafikiaan an mapendekezo ya mwanasheria mkuu Jeff Sessions kwamba "hauwezi kuongoza vyema idara hii ya uchunguzi wa jinai".
Bw Sessions alisema wizara ya haki imejitolea kudumisha nidhamu ya hali ya juu, uwajibikaji na utawala wa sheria na kwamba "mwanzo mpya unahitajika".
Wengi wameeleza kushangaa kwao kwamba Bw Comey amefutwa kwa jinsi alivyoshughulikia uchunguzi kuhusu barua pepe za Bi Clinton, ikizingatiwa kwamba Bw Trump mwenyewe alimsifu kwa jinsi alivyofuatilia na kuongoza uchunguzi huo.
0 Comments