Nchini Rwanda wagombea wa kiti cha urais katika uchaguzi utakaofanyika mwezi wa 8 wanazidi kujitokeza. Diane Rwigara ametangaza rasmi nia yake ya kugombea urais.
Huyu ni Binti wa mfanyabiashara maarufu wa Kinyarwanda Assinapol Rwigara aliyefariki miaka 2 iliyopita katika mazingira ambayo familia yake ilisema ni tatanishi.

Mgombea huyo wa kiti cha urais amesema anataka kukomesha uonevu na kuleta haki na uhuru wa watu kujieleza nchini Rwanda.
Mwanadishi wa BBC Yves Bucyana anasema katika mazungumzo na waandishi wa habari, Bi Diane Rwigara amesema lengo la mkutano huo ni kutangaza rasmi nia yake ya kugombea kiti cha urais katika uchaguzi wa mwezi wa 8 mwaka huu akisema sababu hasa zinazomfanya kupigania kiti hicho.
''Kuna swala la usalama mdogo ambapo baadhi ya watu hutoweka na wengine kuuwawa katika mazingira ya kutatanisha.huwezi kusema kwamba uko katika nchi yenye Amani na usalama wakati watu wanauawa huku wengine wakikimbia nchi," alisema.
Bi Rwagira akijibu maswali kutoka kwa vyombo vya habari
Image captionBi Rwagira akijibu maswali kutoka kwa vyombo vya habari
Ameongezea kwamba Rwanda hakuna uhuru wa watu kutoa maoni yao na ni tatizo kubwa kwa wakosoaji wa serikali, maswala ambayo yeye anataka kubadilisha:
''Siasa isyobagua kabila au tabaka fulani, ambayo inatoa fursa kwa kila Mnyarwanda na kumpa uhuru wa kutoa maoni yake.Nataka kuondoa dhana kwamba mtu akiwa na msimamo tofauti na serikali basi ataitwa adui wa taifa, hiyo nitaipiga vita katika uongozi wangu," alisema bi Rwigara.
Diane Rwigara mwenye umri wa miaka 35.
Ni binti wa marehemu Assinapol Rwigara, mfanyabiashara alifariki miaka 2 iliyopita kutokana na kile kilichoelezwa na polisi kuwa ajali ya barabarani kauli inayokinzana na ile ya familia yake.
Rais wa Rwanda Paul Kagame
Image captionRais wa Rwanda Paul Kagame
Kuhusu hilo, binti huyo amesema tofauti baina ya pande mbili kuhusu kifo cha babake ni miongoni mwa mambo yaliyomshawishi kupigania kiti cha urais ili kukomesha kile alichosema kuwa uonevu.
Huyu ni Mnyarwanda wa tatu kutangaza rasmi nia ya kutaka kugombea urais nchini Rwanda wengine wakiwa ni Bwana Mpayimana Philippe aliyetangaza kuwa mgombea binafsi na Franck Habineza kutoka chama cha Green.