WIZARA ya Maliasili na Utalii imempongeza Rais John Magufuli kwa kununua ndege mbili aina ya Bombardier Q400 na kuipa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na kuinua sekta ya utalii wa nje na ndani kwa kuwapunguzia gharama za usafiri kwa asilimia 50, watalii wanaokuja.

Kwa mujibu wa wizara, sekta ya utalii imeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kwamba kwa mwaka wa fedha 2016/17, mapato ya sekta hiyo yaliongezeka kutoka dola za Marekani milioni 1.9 hadi dola za Marekani milioni mbili.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema kukua kwa utalii na kuongezeka kwa mapato yake kunatokana na kuongezeka kwa watalii wa nje ambapo mwaka 2015 walikuwa milioni 1.1 na 2016 milioni mbili.
Mwaka jana Rais Magufuli alinunua ndege mbili aina ya Bombardier Q400 kutoka Canada na mwezi ujao anatarajiwa kuleta ndege nyingine mbili za ziada. Mwakani Rais anatarajiwa kununua ndege kubwa aina ya Dreamliner yenye uwezo wa kuchukua abiria zaidi ya 270 kufanya usafiri wa anga nje ya nchi uwe wa uhakika.
Bunge wampongeza JPM
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2017/18 jana, Profesa Maghembe alimpongeza Rais kwa kununua ndege hizo lakini akaonya, bado kuna changamoto ya kukosa usafiri wa moja kwa moja kutoka masoko makuu ya utalii.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Atashashta Nditiye naye alimpongeza Rais John Magufuli kwa kufufua Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) na kuliwezesha kununua ndege zake lenyewe.
Alisema Bunge linaamini kufufuka kwa ATCL kutachangia kuongezeka kwa watalii watakaokuza biashara ya utalii na kuongeza pato la taifa sekta hiyo ichangie kukuza uchumi.
Aliipongeza serikali kwa kuboresha miundombinu ya utalii barabara, huduma za maji na umeme vinavyovutia watalii wengi kutembelea vivutio vya utalii na kuongeza watalii. Mwenyekiti huyo alisema Serikali pia imekuwa ikiendelea kuboresha upanuzi wa viwanja vya ndege kama vile wa Julius Nyerere (JKIA), Dar es Salaam, Songwe, Mwanza, Kigoma na Kilimanjaro (KIA) vitakavyovutia mashirika ya ndege makubwa kutua na kuongeza idadi ya watalii nchini.
Profesa Maghembe alisema jitihada zilifanywa kupanua wigo wa vivutio vya utalii kwa kuhamasisha wananchi kuanzisha na kuendeleza miradi ya utalii wa utamaduni. “Miradi hiyo imeongezeka kutoka 60 mwaka 2015 hadi miradi 66 mwaka jana,” alieleza Waziri Maghembe.
Alisema kupitia idara ya utalii huduma za utalii zilikaguliwa na 53 zilipata viwango vya nyota tano (moja), nyota nne (mbili), nyota tatu (13), nyota mbili (31) na nyota moja (6).
Maduhuli yaongezeka
Profesa Maghembe alisema maduhuli ya ada za biashara ya utalii yameongezeka kutoka Sh bilioni 4.1 mwaka 2015 hadi Sh bilioni 5.6 mwaka jana, ongezeko la asilimia 36.
Alisema ongezeko hilo limetokana na matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa usajili na utoaji leseni na kampuni za huduma ya utalii kuongezeka kutoka 1,087 mwaka 2015 hadi 1,244 mwaka jana.
Pamoja na mafanikio hayo, Profesa Maghembe alisema sekta hiyo bado ina changamoto za ufinyu wa bajeti, mfumo wa malipo (Visa, Amex, Mastercard), idadi ndogo ya huduma za malazi, mtazamo hasi wa jamii kwa wahudumu wa utalii na gharama za juu za huduma zake.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2017/18, wizara imejipanga kuweka msisitizo kutangaza utalii katika nchi zinazokua kwa haraka siku za karibuni kama Israel, China na Urusi.
Ujangili wadhibitiwa
Alizungumzia ujangili, alisema udhibiti wake umeonesha mafanikio makubwa katika mwaka wa fedha wa 2016/17, ambapo jumla ya watuhumiwa 7,085 walikamatwa kwa ujangili baada ya kuendesha doria ya siku 349,103.
Pia imebainisha kuwa katika jitihada za kuimarisha doria dhidi ya ujangili kwa kutumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani na mbwa maalumu wa kunusa, wahalifu 906 walikamatwa na kati yao 384 walifikishwa mahakamani.
Alisema watu hao waliokamatwa walikutwa na meno ya tembo 129 na vipande 95 vyenye uzito wa kilo 810.03. Alisema vielelezo vinavyohusishwa na ujangili ni pamoja na silaha za kivita 48, silaha za kiraia 150, risasi 1,058, magobori 406, silaha za jadi 22, 307 na roda 120, 537.
“Lakini pia taarifa za kiitelejinsia zinaonesha majangili wakubwa sasa wanakimbilia nje ya nchi kujificha na wengine wanasalimisha silaha kwa hiari yao. Napenda kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa kikosikazi, Polisi na kamati za ulinzi za wilaya na mikoa,” alisema.
Vielelezo vingine vilivyokamatwa ni pikipiki 189, baiskeli 214, magari 20, ng’ombe 79,831 na samaki kilo 4,043. Alisema katika operesheni dhidi ya ujangili, kesi 2,097 zilifunguliwa mahakamani na kesi 802 zilimalizika.
Kesi 262 za watuhumiwa 472 zilimalizika kwa wahusika kufungwa jela miezi 42,153 na k watuhumiwa 79 waliachiwa. Alisema kesi 276 zilimalizika kwa watuhumiwa 469 kulipa faini ya Sh milioni 452.1 na 966 zinaendelea kusikilizwa.
“Pia kwa kushirikiana na Interpol, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania imewakamata vinara wa ujangili wa Uganda, China na Austria. Katika matukio hyayo wanyamapori hai waliokamatwa ni kobe 342,” alieleza.
Hata hivyo, Profesa Maghembe alisema katika kuepusha madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu, doria 935 zilifanyika na mamlaka hiyo iliua wanyama 31 ili kunusuru wananchi na mali zao.
Aliwataja wanyama waliouawa kuokoa watu kuwa ni tembo wawili, fisi 10, mamba watatu, nyani wawili, samba watatu, kiboko watatu, nyati watano na tumbili watatu. Alisema serikali itaendelea kuimarisha ulinzi kwa kulinda wanyamapori dhidi ya ujangili na biashara haramu ikome.
Pamoja na kuendesha doria, serikali pia ilielekeza nguvu zake kuepusha migogoro kwenye hifadhi ambapo Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeweka alama 1,518 kati ya 2,171, asilimia 70 ya mipaka ya hifadhi zake.
Bunge: NGOs zifutiliwe mbali
Kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, imeishauri serikali kuzifuta Asasi zote zisizo za Kiserikali (NGOs) zinazofanya shughuli zake katika Pori Tengefu la Loliondo na kusajili chache kwa masharti na vigezo vya kulinda na kuhifadhi rasilimali za nchi.
Kamati hiyo ilichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa NGOs 25 zilizojikita katika utalii, uhifadhi na utetezi wa wananchi Loliondo, huku nyingi zikiwa zinamilikiwa na wanasiasa na kufadhiliwa na taasisi za kimataifa ambazo kamati hiyo ilisema kuwa haina uhakika wa malengo yake.
Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kuhusu Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka fedha 2017/18, Mwenyekiti wake, Nditiye alisema wamebaini asasi hizo huchangia migogoro kati ya serikali na wananchi huko.
Hata hivyo, kamati hiyo pia iliishauri serikali kuweka wazi masharti ya uwekezaji na uwindaji katika mapori na hifadhi nchini kuondoa migogoro inayoendelea hasa Loliondo. Pia aliishauri serikali kumaliza migogoro ya ardhi katika mamlaka za hifadhi na wananchi wanaozizunguka.
“Kamati inashauri uandaliwe mpango maalumu wa matumizi ya ardhi utakaoainisha maeneo ya hifadhi na mipaka yake na maeneo kwa ajili ya malisho na shughuli nyingine za binadamu kwa lengo la kuwawezesha wafugaji watumie maeneo hayo na si kuvamia hifadhi,” alisema.
Pia waliishauri serikali kuharakisha mchakato wa kufanya maamuzi yenye tija ili kuokoa gharama ambazo serikali inaingia kwa kumtunza Faru Fausta aliye katika uangalizi maalum kutokana na maradhi aliyonayo na umri wake.
Upinzani wanena
Msemaji wa Kambi ya Upinzani bungeni, Esther Matiko alisema, mgogoro wa Loliondo umedumu kwa miaka 30 sasa hali inayoigharimu serikali na maisha ya wananchi.
Aliishauri serikali kuchukua hatua madhubuti za kutatua mgogoro huo kwa kuwarejeshea wananchi wa eneo hilo kilometa za mraba 25,000 kwa ajili yao na mifugo yao. Kauli ya Serikali Katika maelezo yake, Profesa Maghembe alisema serikali inafanya jitihada kubwa za kutatua migogoro ya ardhi kati yake na wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya hifadhi.
Pia alisema kupitia Taasisi ya Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania, utafiti unaonesha mwenendo wa magonjwa yanayoambukiza kati ya wanyamapori, mifugo na binadamu unatokana na kuwepo kwa mwingiliano mkubwa wa binadamu, mifugo na wanyamapori nchini.
Faru John amtesa Maghembe
Akihitimisha, Profesa Maghembe aliwaambia wabunge sakata la Faru John lilimnyima usingizi. “Sakata hilo, lilihusisha maofisa watano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wanaotuhumiwa kushiriki kumwondoa Faru John kutoka Creta ya Ngorongoro.
Bajeti ya maendeleo juu
Katika mwaka wa fedha 2017/18, wizara imeomba kuidhinishiwa Sh bilioni 148.6. Kati yake, Sh bilioni 96.8 n za matumizi ya kawaida na Sh bilioni 51.8 miradi ya maendeleo.
Bajeti hiyo iliyoombwa imeongezeka kwa Sh bilioni 12.8 sawa na asilimia 9.4 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17. Bajeti ya maendeleo imeongezeka kutoka Sh bilioni 17.7 mwaka 2016/17 hadi Sh bilioni 51.8.