Rais wa Marekani Donald Trump ametetea kile alichokitaja kuwa haki yake ya kubadilishana habari na Urusi.
Kupitia mtandao wa Twitter alisema kuwa yeye ana haki kubadilishana habari na maoni na Urusi kwa kuwa taifa hilo lina hamu kubwa ya kuimarisha vita vyake dhidi ya kundi la Waislamu wenye itikadi kali wa Islamic State na makundi mengine ya kigaidi.

Hii ni kufuatia habari zilizochapishwa na vyombo vya habari nchini Mareknai kuwa alihatarisha usalama wa taifa kwa kushauriana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov juma lililopita.
Awali Ikulu ya White House ilikanusha kuwa Bwana Trump aliongea mambo yoyote ya siri na Waziri Lavrov.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Urusi ilikanusha taarifa hizo za habari na kusema kuwa zilikuwa habari za bandia.
Tuhuma kwamba huenda maafisa wa kampeni wa Bw Trump waliwasiliana na maafisa wa Urusi zimegubika utawala wa rais huyo, na kufikia sasa uchunguzi unaendelea.
Wakati wa kampeni, Bw Trump alimkosoa sana mpinzani wake wa chama cha Democratic Hillary Clinton, kwa jinsi alivyoshughulikia taarifa ambazo zinafaa kuwa siri kuu.

Nini hasa kilitokea?

Katika mazungumzo yake na Bw Lavrov pamoja na balozi wa Urusi nchini Marekani katika afisi yake White House, trump alifichua maelezo ambayo huenda yakapelekea kutambuliwa kwa mdokezi aliyetoa habari hizo, maafisa waliambia Washington Post na New York Times.
Walizungumzia njama ya IS. Rais huyo inadaiwa alianza kuzungumzia mambo ambayo alikuwa hajapangiwa kuyazungumza, na kufichua maelezo zaidi kuhusu njama hiyo.
Njama hiyo inadaiwa kujumuisha kutumiwa kwa laptop kwenye ndege. Mazungumzo ya trump yaligusia ni jiji gani kulikuwa kumegunduliwa tishio.
Habari hizo za kijasusi zilitoka kwa mshirika wa Marekani na zilichukuliwa kuwa za usiri mkubwa kiasi kwamba hazikufaa kufahamishwa washirika wengine wa Marekani, magazeti hayo yameripoti.
Wengine waliokuwepo katika mkutano huo waligundua kosa hilo la Bw Trump na wakachukua hatua kujaribu kuzima moto huo kwa kuwafahamisha maafisa wa CIA na maafisa wa Shirika la Usalama wa taifa (NSA), gazeti la Washington Post linasema.
Donald Trump tweet from 2016
Image captionDonald Trump alimkosoa sana Hillary Clinton kuhusu siri za serikali wakati wa kampeni
Hatua ya Bw Trump si kwamba ni kinyume cha sheria, kwani Rais wa Marekani ana uhuru wa kuamua ni habari gani zitaorodheshwa kama siri kuu na gani hazitaorodheshwa kama siri kuu.
Mkutano huo ulitokea siku moja baada ya Bw trump kumfuta kazi mkuu wa FBI James Comey, hatua iliyoshutumiwa vikali kwamba FBI walikuwa tayari wanachunguza uhusiano wa maafisa wa kampeni wa Bw Trump na maafisa wa Urusi.

White House wamesema nini?

Mshauri mkuu wa usalama wa taifa HR McMaster ameambia wanahabari kwamba taarifa hizo, kama zilivyoripotiwa na magazeti hayo mawili, ni za uongo.
"Rais na waziri huyo wa mambo ya nje walizungumza kuhusu hatari mbalimbali zinazokabili nchi hizi mbili, zikiwemo hatari katika sekta ya uchukuzi wa kutumia ndege,2 alisema.
"Haikutokea - hata wakati mmoja - ambapo duru za kijasusi au njia za kupokea habari zilizungumziwa. Na rais hakufichua shughuli zozote za kijeshi ambazo kufikia sasa hazifahamiki na umma."
Kupitia taarifa, Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson alikariri hilo na kusema maelezo ya ndani kuhusu "hatari mbalimbali" hayakuzungumziwa na kwamba wadokezi, njia au operesheni za kijeshi havikujadiliwa.
Gazeti la Washington Post, ambalo lilichapisha habari hizo kwanza, lilisema hilo si kukanusha taarifa hizo.
James Comey.Haki miliki ya pichaREUTERS
Image captionJames Comey alifutwa kazi na Bw Trump
Mwanahabari Greg Jaffe aliambia BBC kwamba gazeti la Post liliweka wazi kwamba rais hakuzungumzia wadokezi wala njia za kupata habari hizo za kijasusi.
Lakini akaongeza: "Taarifa yetu ilizungumzia habari zenyewe ambazo zingewezesha Warusi kurudi nyuma na kufuatilia na kuweza kujua wadokezi na njia zenyewe. Alisema mengi sana kiasi kwamba wanaweza kujua hayo (mdokezi na njia hizo)."