Waziri wa Ulinzi, Dk Hussen Mwinyi
WABUNGE wameungana bungeni kwa kuitaka Serikali kutoa fedha zote za maendeleo za Wizara ya ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili wizara hiyo iweze kutekeleza na kukamilisha mipango yake.
Hoja hiyo iliibuliwa baada ya Waziri mwenye dhamana, Dk Hussein Mwinyi kueleza katika hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/18 kuwa katika bajeti iliyopita, alipokea asilimia 14.5 pekee ya fedha za maendeleo.

Wabunge wengi ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, waliitaka Serikali ilifanyie kazi suala hilo kwa kuhakikisha fedha hizo zinatolewa kwa wizara hiyo.
Mwenyekiti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu, aliitaka serikali kuhakikisha inatoa fedha zote za maendeleo zilizopitishwa katika mwaka wa fedha unaoishia 2016/17 ili wizara hiyo ikamilishe mipango yake.
Wakati hayo yakijiri, Waziri Mwinyi amewahakikishia Watanzania kuwa hali na usalama wa mipaka ya nchi na nchi kwa ujumla ni shwari licha ya kuwepo kwa changamoto za kutotengemaa kwa hali ya usalama kwa baadhi ya nchi jirani na Tanzania.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani iliwasilisha hotuba yake, lakini ililazimika kuondolewa sehemu takribani tano za hotuba hiyo na kuamriwa kutoingizwa kwenye kumbukumbu za Bunge (hasard) baada ya kubainika kwenda kinyume na Kanuni za Bunge.
Hata hivyo, katika hotuba hiyo iliyowasilishwa na Msemaji wa Kambi hiyo kwa wizara hiyo, Mwita Waitara, wapinzani wameiomba serikali kupeleka askari jeshi katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji zinazokabiliwa na mauaji ya viongozi wa vijiji kukabili hali hiyo.
Fedha Kidogo za Maendeleo
Katika hotuba yake hiyo, Mwinyi alibainisha kuwa hadi kufikia Aprili mwaka huu, wizara hiyo kwa upande wa fedha za matumizi ya maendeleo ilipelekewa kiasi cha Sh bilioni 35.9 sawa na asilimia 14.5 ya kiwango cha fedha kilichopitishwa katika bajeti ya mwaka 2016/17 ambacho ni Sh bilioni 248.
Alisema kwa upande wa fedha za matumizi ya kawaida, tayari wizara hiyo imepokea kiasi cha Sh trilioni 1.2 sawa na asilimia 69.1 ya bajeti ambayo ni Sh Sh trilioni 1.5. Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Balozi Adadi, aliitaka serikali kuhakikisha inatoa fedha zote za maendeleo zilizopitishwa katika mwaka wa fedha unaoishia 2016/17 ili wizara hiyo ikamilishe mipango yake.
Aidha, aliitaka Serikali itafute uwezekano wa kutoa Sh bilioni 27 zilizotengwa katika bajeti hiyo inayoishia lakini hadi sasa hazijatolewa kwa wizara hiyo, kwa ajili ya kupima na kulipa fidia kwa maeneo yaliyochukuliwa na jeshi kabla ya Juni 30, mwaka huu.
Awali, akiwasilisha bajeti hiyo, Dk Mwinyi alisema wizara hiyo inaomba kuidhinishiwa jumla ya Sh trilioni 1.7 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Kati ya fedha hizo Sh trilioni 1.5 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh bilioni 219 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.Mwaka 2016/17 wizara hiyo iliidhinishiwa jumla ya Sh trilioni 1.7.
Hali ya Usalama; Waziri Mwinyi, akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti yake, alisema, “Aidha, uwepo wa hali ya matishio ya ugaidi wa kimataifa umevilazimu vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na nchi jirani na raia wake kuendelea kuwa katika hali ya tahadhari na umakini ili endapo kutajitokeza dalili yoyote inayotishia usalama, hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka,” alisisitiza.
Alibainisha kuwa kwa sasa katika maeneo ya ukanda wa Afrika Mashariki, Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika, bado kuna baadhi ya nchi hali ya usalama haijatengemaa ikiwemo nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Somalia na Sudan Kusini.
Alieleza kuwa hali ya mipaka ya nchi yenye jumla ya urefu wa kilometa 5,390 ni shwari ingawa pia kuna baadhi ya mipaka inapakana na nchi zenye migogoro kama vile mpaka wa magharibi unaopakana na nchi za Burundi na DRC.
Alisema pamoja na mpaka huo kuwa shwari umekuwa ukikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kutokamilika kwa mazungumzo ya upatanishi ya pande zinazosigana nchini Burundi hali inayosababisha hali kisualama kutotengemaa.
Pia alisema uwepo wa vikundi vya waasi vyenye silaha vinavyoendesha harakati za kimapigano dhidi ya majeshi ya DRC na majeshi ya Umoja wa Mataifa (MUNUSCO), kunasababisha ongezeko la wakimbizi hali inayohatarisha usalama kwenye eneo la mpaka huo.
Alibainisha kuwa jeshi hilo limeendelea la jitihada za kuimarisha usalama wa mipaka hiyo hatua inayochangia kudhibiti na kupunguza matukio na vitendo vyenye kutishia usalama kama vile ugaidi, biashara ya dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu, uhamiaji haramu na ujambazi.
Alisema jeshi hilo limeshiriki Operesheni Amboni 2 mkoani Tanga iliyoanza Mei, mwaka jana na kufungwa rasmi Desemba mwaka jana wahalifu hao walidhibitiwa. Aidha, Dk Mwinyi alisema jeshi hilo pia linaendelea kushiriki katika operesheni za ulinzi wa amani chini ya UN na Umoja wa Nchi za Afrika AU ambapo imepeleka vikosi vyake Darfur nchini Sudan.
Alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 JKT imefanikiwa kuendesha mafunzo kwa vijana 14,748 wa mujibu wa Sheria, kati yao wavulana ni 10,863 na wasichana 3,885 waliohitimu kidato cha sita mwaka jana idadi ambayo ni sawa na asilimia 73.7 ya lengo la kuchukua vijana 20,000.
Hotuba ya Upinzani; Kuhusu hotuba ya upinzani, wakati Waitara akisoma hotuba hiyo jana bungeni, mara kadhaa mbunge wa Newala, George Mkuchika ambaye pia ni Kapteni Mstaafu aliomba miongozo na kuikosoa akieleza kuwa imejaa maneno ya siri ambayo hayapaswi kubainishwa hadharani lakini pia mengine itakuwa vigumu kwa kambi hiyo ya upinzani kuyathibitisha.
Waitara akiwasilisha maoni ya kambi hiyo ya upinzani, kuhusu bajeti ya Wizara hiyo, alizungumzia baadhi ya maeneo ikiwemo amri ya kuongezewa muda wa kazi wa askari jeshi na majukumu ya Mkuu wa Majeshi (CDF) jambo ambalo halipaswi kuzungumzwa na yeye.
Maeneo mengine ambayo yalifutwa ni pamoja na eneo la kumdhihaki Rais John Magufuli kuhusu agizo lake la kulitaka Shirika la Umeme (Tanesco) kuwakatia umeme wale wote watakaoshindwa kulipa madeni yao na maeneo mengine ambayo yalifutwa mapema kwa amri ya Spika wa Bunge Job Ndugai kutokana na kukiuka kanuni za Bunge.
Akitoa majibu ya mwongozo huo Zungu alikubaliana na Mkuchika na kuamuru maeneo yote yaliyoainishwa na mbunge huyo kwenye hotuba hiyo yasisomwe bungeni hapo na yaondolewe kwenye kumbukumbu za hansard.
Awali, kabla ya hotuba hiyo kusomwa, Zungu alisoma maelekezo ya Spika Ndugai ya kufuta maeneo mawili ya sehemu za hotuba hiyo baada ya kubainika kuwa yanakiuka kanuni za Bunge.