DAR ES SALAAM: Wapenda ubuyu wanakuambia hakuna kinachodumu milele duniani! Ndiyo maneno unayoweza kusema kutokana na maisha ya Mshindi wa Big Brother Africa (BBA) mwaka 2014, Idris Sultan ambayo anaishi kwa sasa.
Kwa mujibu wa watoa ubuyu, maisha ya jamaa huyo ni tofauti kabisa na matarajio ya wengi kutokana na mshiko aliovuta BBA wa zaidi shilingi milioni 500 za Kibongo.
NDIYO CHOKA MBAYA?
Inasemekana kuwa, ishu hiyo ndiyo ilizua maswali kwa watu wake wa karibu wakihoji ndiyo jamaa amekuwa choka mbaya? Vyanzo makini vililiambia Wikienda kuwa, kwa sasa Idris anaonekana amechoka mbaya kwani anadaiwa kuhama kwenye jumba la ghorofa alilokuwa akiishi Mbezi-Beach jijini Dar na kuhamia kwenye chumba kimoja maeneo ya Mbezi-Chini, Dar.
“Kiukweli maisha anayoishi Idris yanashangaza sana na inaonekana ameshamaliza zile shilingi milioni mia tano alizoshinda BBA.“
Inaonekana zimekata maana siyo wa kwenda kupanga chumba kimoja wakati mwanzoni kabisa baada ya kushinda alikuwa anaishi kwenye ghorofa na maisha yake yalikuwa ya mwendokasi (kufuru ya fedha) kwa kuwa mkwanja ulikuwepo.
“Kwa sasa anaishi maisha ya kawaida kama vile hajawahi kupata fedha nyingi kiasi kile. “Sasa sijui alizimalizia wapi fedha zote zile au aliendekeza sana bata maana vijana wengi wa Dar wanapenda kujiachia wanapopata fedha huku wakiendekeza tabia ya kubadilisha totozi kila kukicha,” kilisema chanzo chetu kwa sharti la kutotajwa gazetini.
OFM WAMFUNGIA KAZI
Baada ya kupata ubuyu huo, kikosi kazi cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) kilicho chini ya Global Publishers kilimfungia kazi Idris ambapo walifika Mbezi-Chini anakodaiwa kuishi kwenye chumba kimoja.
MAJIRANI WAFUNGUKA
Walipofika anakoishi, OFM walijifanya wageni wake, lakini wapangaji wenzake walidai kuwa alitoka. Hata hivyo, jibu hilo liliwathibitishia OFM kuwa Idris anaishi pale ambapo walipata fursa ya kuoneshwa mlango cha chumba chake.Mazingira ambayo OFM ilishuhudia ni tofauti na maisha aliyokuwa akiishi awali ambapo ilibidi kufotoa picha kadhaa.“Ni kweli hapa ndipo anapoishi Idris kwa upande wa mbele wa nyumba hii lakini kwa sasa hayupo, naona ameenda kazini (kwa sasa ni Mtangazaji wa Choice FM na ni msanii wa vichekesho,” alisema jirani mmoja aliyeomba hifadhi ya jina ili asije akaonekana ‘mnoko’ na kutibua ujirani mwema na staa huyo na kuongeza:
“Lakini ni mtu mzuri na tunafurahi kuishi na staa.”
IDRIS ASAKWA
Baada ya kumkosa nyumbani hapo, OFM walimsaka Idris kwa njia ya simu lakini iliita bila kupokelewa.
Hata hivyo, baadaye alituma ujumbe mfupi kwamba atumiwe meseji ambapo mazungumzo yalikuwa hivi;
OFM: Kuna habari kwamba kwa sasa umefilisika na unaishi kwenye chumba kimoja, tofauti na mwanzo ulivyokuwa unaishi kwenye ghorofa la ukweli, hii ishu ikoje?
Idris: Haahaaa..! Hivi nina endorsements (mikataba ya madili) ngapi? Ukipiga hesabu ukakadiria utakuwa unajua nina thamani gani. Ila unaruhusiwa kuhisi vingine.
OFM: Sawa, lakini sisi ni vijumbe tu. Mashabiki wako wanataka uweke wazi kuhusu fedha ulizopata ziliishia wapi ili kumaliza maneno yanayozungumzwa?
Idris: Huwezi kuzuia watu kuzungumza ndugu yangu. Nikianza kuwaza mangapi ya kuyaweka wazi, nitajikuta ninajieleza kutwa kucha.
NENO LA MHARIRI
Sisi kazi yetu ni kumfikishia ubuyu mhusika na ndicho tulichokifanya lakini ni vizuri Idris akaweka mambo hayo wazi kwa sababu shilingi milioni 500 kukata kwenye mazingira kama hayo kunazua maswali mengi.
|
0 Comments