|
MKOA wa Kilimanjaro umetajwa kuwa ndio mkoa unaoongoza nchini kwa uzalishaji wa mihadarati ukifuatiwa na Mkoa wa Arusha.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya (DCEA), Mihayo Msikhela, katika Mkoa wa Kilimanjaro, Wilaya ya Same ndio inayoongoza kwa uzalishaji huo wa mihadarati.
Msikhela aliyasema hayo katika operesheni ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya iliyofanyika jana wilayani Same. Alisema kuna mikoa mitano inayoongoza kwa kilimo cha mihadarati nchini ikiwemo mikoa ya Kagera, Songwe na Tanga, lakini wilayani Same katika maeneo ya Chome na Suji ndio yanayoongoza kwa kilimo hicho cha mihadarati.
Alitaja maeneo mengine wilayani humo yanayolima mihadarati ikiwemo bangi na mirungi kuwa ni vijiji vya Tae, Ekonte na Rikweni ambako kuna jumla ya ekari 48 zilizoharibiwa za mihadarati.
Kamishna huyo alisema DCEA ambayo inafanya kazi kwa ukaribu na polisi, itahakikisha inafikia mikoa yote nchini ili kuharibu mashamba yote yanayozalisha mihadarati hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kuanza kuachana na kilimo cha mihadarati na badala yake wajikite zaidi katika kilimo cha chakula na mazao ya biashara kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Alisema wilaya hiyo inapoteza eka nyingi zenye rutuba na saa nyingi za nguvukazi kwa kuwa baadhi ya wananchi katika wilaya hiyo wamekuwa wakitumia nguvu na muda kulima bangi na mirungi badala ya mazao yenye faida kwao.
0 Comments