Katika hatua iliyowashangaza wengi nchini Rwanda vyama viwili vya siasa vikongwe nchini humo vimemtangaza Rais Paul Kagame kuwa mgombea wao katika uchaguzi wa urais utakaofanyika mwezi wa 8 mwaka huu, kabla hata chama chake cha RPF kumtangaza kuwa mgombea wake.

Hadi sasa ni wagombea binafsi 3 waliokwishatangaza nia ya kusimama katika uchaguzi huo.
Katika mikutano mikuu ya vyama hivyo, chama cha Social Democratic na Liberal Party licha ya kwamba ilifanyika mnamo nyakati tofauti, kauli yao ilikuwa moja, kuunga mkono Rais Paul Kagame wa chama tawala cha RPF katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi wa 8 mwaka huu.
Uchaguzi mkuu unafanyika Rwanda mwezi wa 8 mwaka huu
Image captionUchaguzi mkuu unafanyika Rwanda mwezi wa 8 mwaka huu
Hoja iliyotolewa na vyama hivyo pia haitofautiani.
Ni kwamba chaguo lao limetokana na pendekezo lililoungwa mkono na wananchi wengi wa Rwanda la kubadili katiba na kumpa rais Paul Kagame uhuru wa kugombea muhula wa tatu kupitia kura ya maoni iliyopitisha katiba mpya mwaka jana.
Haya yametokea wakati ambapo hata chama tawala RPF hakijamtangaza Rais Paul Kagame kama mgombea wake, wakati mchakato wa uteuzi bado umekuwa ukiendelea katika ngazi ya mashinani.
Wengi walitarajia kuwa vyama hivi vingeteua na kutangaza wagombea wake katika uchaguzi huo kama ilivyotokea katika uchaguzi wa urais mwaka 2010.
Chama cha Social Democratic kilisimamiwa na Dr Jean Damascene Ntawukuriryayo aliyepata asilimia 4,9 ya kura ilhali Liberal Party kilisimamiwa na Higiro Prosper aliyeambulia asilimia 1 nukta 3 ya kura.