Watu takriban 10,000 wamelazimika kukimbia makwao kutoka mji mmoja pwani ya Afrika Kusini ambao umeharibiwa pakubwa na moto.
Wanajeshi wanashiriki katika juhudi za kukabiliana na mtaa huo kukabili moto huo ambao unawaka katika maeneo 25 katika mji wa Knysna.

Watu wanane wamefariki kutokana na upepo mkubwa na moto ambao umekumba mji huo na maeneo mengine katika kanda ya Cape Magharibi.
Upepo huo mkubwa umesaidia kueneza moto huo.
Nyumba zaidi ya 150 zimeteketezwa eneo hilo kwa mujibu wa shirika la wazimamoto.
Mji huo una takriban wakazi 77,000.
Unapatikana kilomita 500 mashariki mwa mji wa Cape Town.
FiresHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionKnysna ni maarufu sana kwa watalii
Jeshi la Taifa la Afrika Kusini litasaidia kuangusha mabomu ya maji yanayotumiwa kuzima moto kusaidia kukabili moto huo, msemaji wa jeshi Simphiwe Dlamini amesema.
Wanajeshi karibu 150 watatumwa eneo hilo kuzuia wahalifu kupora mali katika maeneo ambayo wenyewe wamekimbia.
Mwezi Mei, mkoa wa Cape Magharibi ulitangaza janga ya ukame baada ya mabwawa mawili makubwa kukauka kabisa.
Ukame huo unadaiwa kuwa mbaya zaidi kukumba eneo hilo katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.
Mataifa mengine Afrika kusini yamekabiliwa an ukame wa zaidi ya miaka miwili, unaotokana na hali ya hewa ya El Nino.
Hata hivyo, maeneo mengine yamepata mvua kwa wingi na mavuno ya mahindi kuongezeka.