Zimbabwe imeuza ng'ombe wa thamani ya $1m (£770,000) kwenye mnada na kukabidhi pesa hizo kwa Wakfu wa Muungano wa Afrika kusaidia kumaliza utamaduni wa kutegemea fedha kutoka kwa wafadhili wa nje, Rais Robert Mugabe amesema.

Rais huyo amesema binafsi alitoa ng'ombe 300 kutoka kwa zizi lake, nao raia wengine wa Zimbabwe wakaongeza ng'ombe wengine kiasi sawa na hicho.
Bw Mugabe alikabidhi hundi ya $1m kwa AU wakati wa mkutano mkuu wa viongozi wa mataifa wanachama nchini Ethiopia.
Mchango huo wa Zimbabwe umetokea kipindi ambacho taifa hilo linakabiliwa na uhaba wa fedha na chakula.
Mwaka jana, watu zaidi ya milioni nne nchini humo walihitaji chakula cha msaada baada ya mvua kutonyesha vyema.
Hata hivyo, mwaka huu mavuno yamekuwa tele na taifa hilo linatarajiwa kujitosheleza kwa chakula kwa mara ya kwanza katika miaka mingi.
Upinzani umelaumu serikali kwa uhaba huo wa chakula, na kusema kwamba sera yake yenye utata ya kupokonya wazungu mashamba ilichangia kusambaratisha sekta ya kilimo.
Zimbabwe imelazimika pia kuanza kutumia hati za dhamana baada ya kuishiwa na dola za Marekani, pesa ambazo hutumiwa kwa biashara nchini humo.
Kiwango cha juu cha mfumko wa beii kiliilazimu Zimbabwe kuacha kutumia dola yake mwaka 2009.
Waziri wa mambo ya nje Simbarashe Mumbengegwi amesema ng'ombe hao sana walitolewa na watu waliofaidi kutokana na mageuzi katika sera ya mashamba nchini humo, kwa mujibu wa gazeti la serikali la Herald.
Msaada huo ulikuwa ni "kuimarishwa" kwa ahadi ya Bw Mugabe ya mwaka 2015 kwamba angetoa ng'ombe 300.
Akiongea katika mkutano huo, Bw Mugabe alisema mchango huo ni mdogo tu lakini ni ishara muhimu katika kujaribu kukomesha utegemezi wa Afrika kwa pesa za wafadhili.
Robert MugabHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Image captionRobert Mugabe, 93, ametawala Zimbabwe tangu 1980
"Kama Mwafrika na mkulima, kutoa ng'ombe ni jambo la kawaida kwangu, ikizingatiwa kwamba bara letu limebarikiwa na ng'ombe wengi na ng'ombe hutazamwa kama hazina ya utajiri," Bw Mugabe alisema.
Kwenye tovuti yake, Wakfu wa AU unasema huwa unaangazia mipango ya vijana na wanawaje, na kuendeleza usawa wa jinsia.
Wakati wa kipindi chake kama mwenyekiti wa AU kati ya 2015 na 2016, Bw Mugabe alitetea AU iwe ikifadhiliwa na Waafrika.
Kwa sasa asilimia 60% ya bajeti ya umoja huo hutoka kwa wafadhili kutoka nje.