|
SERIKALI imetoa ufafanuzi kuhusu matamshi iliyoyaita ya kichochezi na yenye kuudhi, yaliyotolewa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kuwa inabana demokrasia na kusema kuwa matamshi hayo ni propaganda zilizoendeshwa kwa minajili ya kisiasa.
Aidha, imemshauri Lissu ambaye pia ni Wakili wa Mahakama Kuu, kufanya kazi yake kwa weledi na kusimamia maadili na si kuupotosha umma kwa sababu zake za kisiasa. Katika taarifa aliyoitoa kwa umma jana, Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dk Hassan Abbas, alisema matamshi ya Lissu yalinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari juzi, pia yalikejeli Mahakama.
Kwa mujibu wa Dk Abbas, serikali itaendelea kuenzi na kuilinda misingi ya demokrasia, uhuru wa watu na kuwapa fursa wananchi kushiriki katika uchumi wa nchi hasa wakati huu wa mageuzi makubwa ya kiutendaji chini ya Rais John Magufuli.
Hata hivyo, alisema “Lakini serikali haitavumilia mtu yeyote au kikundi chochote kitakachojaribu kutumia uhuru wowote vibaya ili tu kukwaza azma hiyo ya Taifa”. Alimuasa Lissu pamoja na wananchi kwa ujumla, kujiepusha na propaganda, kejeli na uzushi usio na msingi dhidi ya serikali au taasisi zake.
Zaidi, alitoa mwito kwa Lissu na wananchi kwa ujumla kutafuta haki kupitia mkondo wa sheria, badala ya kuvunja sheria, ikiwa wataona kuna haki zimekiukwa. Alifafanua kwa nini alichotamka Lissu ni propaganda za kisiasa na kusema alichanganya kati ya haki katika demokrasia, ambazo hata yeye amezitumia kuzungumza na wanahabari bila tashtiti kwa upande mmoja na misingi ya wajibu kwa upande mwingine ambayo kila mmoja, iwe Tanzania au kwingineko duniani, anayo na pale anapokiuka hatua huchukuliwa.
Alisema tofauti na upotoshaji wa Lissu, Tanzania ikiwa nchi kiongozi Afrika na duniani katika kuenzi demokrasia na kupigania haki, si tu inaendelea kuenzi misingi hiyo, bali pia imechukua hatua za wazi kuhakikisha kuwa misingi hiyo inalindwa na pale mtu na hata taasisi zinapokiuka, mkondo wa sheria huchukua nafasi yake.
“Ikiwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), Tanzania imeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 na huwasilisha taarifa zake za utekelezaji wa demokrasia na haki za binadamu katika Kamisheni ya UN ya Haki za Binadamu,” alisema Dk Abbas.
Pia, alieleza kuwa Kikanda, Tanzania ikiwa mwanachama kiongozi wa Umoja wa Afrika (AU) imeridhia Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na ni miongoni mwa nchi za kwanza Afrika kukubali kushtakiwa na wananchi wake kwa kuridhia itifaki ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na pia kukubali kufanyiwa ukaguzi katika utawala bora kupitia Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
Kitaifa, pamoja na kuruhusu taasisi anuai za umma na binafsi, Dk Abbas alisema Serikali ya Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache Afrika yaliyotunga sheria ya ndani ya nchi inayowapa wananchi wake haki ya kuishitaki serikali au watu wengine wanapoona wamevunjiwa haki zao za kidemokrasia au kibinadam
0 Comments