WABUNGE wameuchambua Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017, na kuonesha hofu kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo usalama wa madini yatakayohifadhiwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kabla ya kuuzwa.
Wakichangia muswada baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kuuwasilisha katika kamati, wameitaka serikali kuhakikisha inajipanga katika ulinzi kwenye madini. Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM) aliishauri serikali kabla ya kuanza kutumika kwa sheria hiyo, kuongeza ulinzi BoT. “Serikali hii ina vyombo vya ulinzi na usalama vya kutosha, Sheria itakavyoanza kutumika iangalie uwezekano wa kuongeza ulinzi wa kutosha katika Benki Kuu kwa sababu ndio eneo tunalolitegemea,” alieleza.
Naye Mbunge wa Tarime Mjini, John Heche (Chadema) alisema huko nyuma BoT iliwahi kuungua na kuhoji wameangaliaje ili Watanzania wasijeingia katika matatizo. Katika kuonesha hofu yake, Mbunge wa Newala Vijijini, Rashid Akbar (CCM) alisema, “hapo awali BoT iliwahi kutunza dhahabu na mwishowe ziliyeyuka na kuwa mchanga, wasiwasi wangu ni mkubwa kwa sababu dhahabu ni rahisi kuibwa.
Ni vema serikali ikachukua ulinzi kutoka nje.” Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almasi Maige (CCM) alihoji utaalamu wa BoT katika utunzaji wa madini kwani utunzaji wa maliasili hiyo haufanani na wa fedha. Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka (CCM), alihoji ushirikishwaji wa wataalamu kutoka nchi ambazo zimeshatekeleza mfumo ambao unakwenda kutekelezwa kupitia sheria ambazo wanaziboresha ili kuzuia wizi.
Mbunge wa Moshi Vijijini, Antony Kom (Chadema) alihoji kama wameangalia uzoefu kutoka nchi nyingine kabla ya kuandika muswada huo ili kuepuka na kukimbiwa na wawekezaji, huku Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi (CCM) akisema muswada huo unakwenda kuunda chombo cha kusimamia madini na kushauri kiwe na vitendea kazi kama Mamlaka ya Mapato (TRA).
Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda (CCM) alisema muswada huu uweke wazi juu ya kufutwa kwa baadhi ya miundo katika Wizara ya Nishati ya Madini. “Kwa jinsi muswada huo ulivyo unahamishia shughuli zote za kamishna wa madini kwa ofisa mtendaji mkuu wa kamisheni itakayoundwa,” alieleza. Kwa upande wake, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM) alisema serikali isijifunge katika ushiriki wa asilimia 16 katika shughuli zote za madini na badala yake tusogee mbele kwa njia ya majadiliano tutakayofanya.
Akijibu hoja hizo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Profesa Florence Luoga aliwaondoa hofu wabunge kuwa katika suala la bima utekelezaji wake hauhitaji kuwa na kampuni za bima za kimataifa kwa kuwa uwekezaji unafanyika nchini. Kuhusu hoja ya kampuni ya madini kulazimishwa kuwa na akaunti nchini, Luoga alisema hiyo ni hoja ya kukuza uchumi.
“Hii itaongeza uwezo wa benki zetu, ingawa pia wana haki na gawio lao na pia wanaweza kuweka katika akaunti za nje,”alisema huku akiongeza kwa kuwataka wabunge na Watanzania kutowafurahisha wawekezaji hadi wakajidhulumu,” alieleza Profesa Luoga. Naye Profesa Kabudi aliwaondoa hofu wabunge kuhusu usalama huku akielezea kuwa wakati BoT inaungua jengo lilikuwa limejengwa kwa mbao tofauti na jengo la sasa ambalo limewekewa teknolojia ya utambuzi wa moto na kuimarisha ulinzi.
Kuhusu hoja ya ripoti za makinikia kupelekwa bungeni, Kabudi alisema ripoti hizo ni mali ya Rais John Magufuli na kwamba labda mwenyewe atake kufanya hivyo. “Wanaotaka wanaweza kwenda kusoma muhtasari, lakini haziwezi kuletwa hapa, labda rais mwenyewe atake,” alieleza. Aidha, Kabudi alisema baada ya kukamilisha sheria ya madini, baadaye watakuja katika sheria za gesi na mafuta.
|
0 Comments