Wafanyakazi wa Bodi ya Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar wakishusha bidhaa zilizoharika katika Dampo la Kibele tayari kwa kuangamizwa.
Moja ya gari lililobeba mchele ulioharibika likishushwa na Wafanyakazi wa Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar katika Dampo la Kibele Mkoa Kusini Unguja.
Gari la kijiko kutoka Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano likiangamiza mchele tani 27.5 ulioharibika katika Dampo la Kibele Mkoa Kusini Ungua.
Picha na Makame Mshenga.



Na Ramadhani Ali – Maelezo 

Wafanyabiashara wa Zanzibar wanaoagiza bidhaa kutoka nje wametakiwa kuwa waadilifu na kuwahurumia wananchi wenzao wakati wanaponunua bidhaa kwa kuangali ubora na kuacha tabia ya kuchukua bidhaa dhaifu zenye bei ndogo kwa lengo la kutafuta faida kubwa.

Mkuu wa Kitengo cha ufuatiliaji madhara ya chakula kutoka Bodi ya Madawa na Vipondozi Zanzibar Bibi Aisha Suleiman alitoa ushauri huo wakati bodi hiyo ilipofanya zoezi la kuangamiza tani 27.5 za mchele ulioharibika na chakula mchanganyiko kilo 400 kilichomaliza muda ikiwemo tende na juice katika Dampo la Kibele Mkoa Kusini Unguj.

Bi. Amina ambae alikuwa msimamizi mkuu katika zoezi hilo alisema mchele ulioharibika uliingizwa nchini na Kampuni ya Zenj General Machandise na uliingia maji wakati wa kusafirishwa na chakula kilichomaliza muda wa matumizi kiligundulika katika maduka mbali mbali ya Zanzibar baada ya kufanyika ukaguzi katika maduka hayo.

Alisema kwa mujibu wa sheria bidhaa zinapoharibika wakati wa kusafirishwa na ikagundulika wakati wa ukaguzi bandarini kabla ya kuingia sokoni mmiliki wa bidhaa hiyo huwa hanakosa na hulazimika kutoa gharama za kuangamiza bidhaa hiyo yeye mwenyewe.

Alisema Kampuni ya Zenj General Machandise ilikubali kutoa gharama ya kuangamiza mchele huo na kazi hiyo imefanyika chini ya usimamizi wa Bodi ya Chakula Dawa na Vipodozi.

Alikumbusha kwamba wananchi wanapotumia chakula kibovu kilichopitwa na wakati wanapata madhara makubwa ikiwemo maradhi hatari ya kensa ambayo matibabu yake yanagharama kubwa na yanapoteza maisha ya wananchi wengi.

Ameongeza kuwa athari ya kutumia chakula kibovu inaweza kuonekana katika kipindi kifupi tu baada ya kula lakini athari nyengine inaweza kuchukua miaka mingi kugundulika.

Hata hivyo amewashauri wananchi kwa upande wao kuwa waangalifu wakati wa kununua bidhaa za chakula na kuhakikisha kuwa bidhaa wanazochukua zinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.