Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe Dkt Dk Charles Tizeba akisisitiza jambo kabla ya kufungwa kwa Maonesho ya Nanenane katika viwanja vya
Ngongo, Manispaa ya Lindi leo tarehe 8 Agosti 2017.





Na Mathias Canal, Lindi

Serikali imesema kuwa  Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi itaendelea
kuwa muhimili na kichocheo katika kujenga uchumi wa viwanda ambao ndio
kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt John
Pombe Magufuli. 

Hayo yalibainishwa na Waziri wa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Dkt Charles Tizeba  wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi Makamu wa
Rais Mhe Samia Suluhu Hassan katika kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya
wakulima, nane nane kitaifa, katika viwanja vya ngongo katika manispaa ya lindi
jana tarehe 8/8/2017.

Dkt Tizeba alisema kuwa kwa
ushirikiano na Watumishi wote katika Wizara, amejipanga kuhakikisha kuwa, Sekta
ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inaendelea kukua sawa sawa na mahitaji ya Wananchi. 

Alisema kuwa jambo hilo linawezekana
ambapo inawezekana kwa kiasi kikubwa kuzalisha malighafi za kutosha za
kuwezesha viwanda kuzalisha bidhaa mbalimbali, ambazo zitauzwa ndani na nje ya nchi
kwa bei nzuri na ya ushindani. 

Alisema kuwa kupitia mbinu hiyo
wizara itakuwa imefanikisha kuongeza mchango wa Sekta hizo katika uchumi wa Taifa
na pia katika kuondoa umaskini kwa Watanzania wengi.

Sambamba na hayo pia Mhe Dt Tizeba
alisema kuwa Sekta ya Kilimo, Mifugo
na Uvuvi inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo, mabadiliko ya
tabianchi, ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia kupungua kwa uzalishaji na tija
ya mazao, uhaba wa malisho ya mifugo na rasilimali maji.  

Katika kukabiliana na jambo hilo
Mheshimiwa Dkt Tizeba alisema kuwa Wizara yake imejipanga kuendelea, kukabiliana
na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na kuzalisha mbegu
bora zinazovumilia ukame, magonjwa na kutoa mavuno mengi. 

Alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana
na Wabia wa Maendeleo, wamekamilisha Mpango wa Kilimo Kinachohimili Mabaliliko
ya Tabianchi na Miongozi ya uzalishaji mazao, ufugaji na uvuvi. Muongozo wa
kilimo umetolewa kulingana na Kanda za Kilimo za Kiteknolojia. Miongozo hiyo, imezinduliwa
na kuanza kusambazwa kwa Maafisa Ugani wa Kilimo Mifugo na Uvuvi na kwa
wananchi, kuanzia Mwezi, Mei na Juni, 2017. 

Alisema Mikakati mingine, inayoendelea
ni pamoja na kuhakikisha kuwa mbolea bora, inapatikana kwa wingi na kwa bei
nafuu zaidi, sawasawa na agizo la Makamu wa Rais la kuwasaidia Wakulima,
Wafugaji na Wavuvi kupunguza gharama za uzalishaji ili waweze kufaidika na
matunda ya juhudi zao.   

Sambamba na hilo aliongeza kuwa
wizara yake imejipanga ili kuhakikisha kuwa inaendelea kuwaelimisha na
kuwasaidia Wafugaji wa Tanzania, kufuga kitaalamu zaidi ili kuepuka hali ya kuhamahama
kwa ajili ya kutafuta malisho na maji. 

Alisema kuwa jambo hilo litawezesha
kufuga kwa tija na pia kupunguza migogoro ya Wakulima na Wafugaji.

MWISHO