Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete
RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ni miongoni mwa watu walihudhuria ibada na maziko ya bilionea Faustine Meleo Mrema (64), yaliyofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto wilayani Arumeru mkoani Arusha; akizikwa katika jeneza na kaburi vilivyogharimu Sh milioni 85.

Msafara wa Mrema aliyefariki dunia Julai 30, mwaka huu katika Hospital ya Garden City nchini Afrika Kusini akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya mifupa, ulianza saa 3.30 asubuhi jana kwa gari jeusi la kisasa aina ya Toyota Landcruiser Vx V8 lenye namba za usajili T 802 DAC.
Msafara huo mkubwa wa magari meusi ya aina hiyo, yalikuwa zaidi ya 180 na mengine kadhaa yaliyopita katika barabara ya Afrika Mashariki kuelekea barabara ya Moshi hadi Ngurdoto, ambako Mrema alikuwa akimiliki hoteli hiyo ya kifahari ya Ngurdoto. Jeneza la milioni 85/- Kwa mujibu wa Gibson Matinga, jeneza lililobeba mwili wa Mrema na kaburi lake vimegharimu zaidi ya Sh milioni 85, ambazo ni fedha zilizochangwa na marafiki zake waliokuwa wakiongozwa na Mwenyekiti wa familia, mfanyabiashara maarufu jijini Arusha na mji wa Moshi, Vincent Laswai.
Matinga alisema kabla ya kifo chake, Mrema alimwachia mali zenye thamani ya mabilioni ya fedha na wosia binti yake, Joan Mrema (23) kusimamia kila kitu zikiwemo biashara zake zilizo chini ya kampuni yake ya Impala Group kwa kumwelekeza nani anapaswa kufanya naye kazi ili shughuli ziendelee bila ya wasiwasi kwa usimamizi wake. Ibada ya misa iliongozwa na Askofu wa Kanisa la International Evangelism Church, Askofu Issangya aliyesema Mrema ni mfanyabiashara wa aina yake mkoani Arusha kwani alikuwa akishirikiana na kila mtu bila ya kujali rangi, dini wala kabila na alikuwa akisaidia kila mmoja na hasa watoto yatima.
Askofu Issangya alisema bilionea huyo alikuwa akiitwa jina la utani “Ofisa” enzi za uhai wake kwani alikuwa mtu msafi na mwenye kujipenda na mchapakazi na asiyetaka makuu, hivyo watu wanapaswa kuiga mafano huo na kuutumia utajiri kwa kuwasaidia wengine wasiokuwa na uwezo. Gambo amlilia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo akizungumza kwa niaba ya viongozi wote wa vyama na serikali mkoani Arusha, alisema Mrema enzi za uhai wake alichangia sana huduma za jamii mkoani humo kutokana na biashara zake na ajira kwa wakazi wake.
Gambo alisema serikali mkoani Arusha imeguswa na kusikitishwa sana na kifo chake, kwani imekosa mtu muhimu sana Arusha na Taifa kwa ujumla. Msemaji wa familia Akizungumza kwa niaba ya familia ya Mrema, mfanyabiashara Laswai alisema familia imeondokewa na mtu muhimu ambaye pengo lake kuliziba itachukua muda mrefu. Laswai aliwashukuru wale wote walioshiriki kumuuguza, kuomboleza na hatimaye kumzika kwani Mwenyezi Mungu atawalipa kwa moyo wa kujitoa waliouonesha kwa familia.
Msemaji wa Impala Group Naye Mattasia Ole Laizer ambaye ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya Impala Group, alisema kumuenzi marehemu ni kuendeleza mema yote aliyokuwa akiyafanya na kwa ushirikiano mkubwa na familia aliyoiacha. Laizer alisema wafanyakazi wa kampuni hiyo walimpenda sana mkurugenzi wao, lakini Mungu amempenda zaidi na wao hawana jinsi ya kufanya na kilichobaki kwao ni kuendeleza miradi yote, aliyoacha bila ya kuwa tatizo lolote.
Mrema ameacha mke na watoto kadhaa na mazishi yake yalikamilika saa 10.30 jioni na watu walikuwa na kunywa katika Hoteli ya Ngurdoto. Wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, wabunge Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Godbles Lema (Arusha Mjini) na Gibson Meseyeki (Arumeru Magharibi), Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro, Balozi mstaafu Daniel Ole Njoolay, Basil Mramba na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti.