Wito wa rais wa zamani wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete kwa vyama tawala barani Afrika kutowachukulia viongozi wa upinzani kuwa maadui na badala yake kuwafanya kuwa washirika wakuu umeungwa mkono na wengi.

Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa Afrika Kuhusu uongozi bora na sheria uliofanyika mjini Johannesburg, Kikwete alitoa changamoto kwa vyama vya kisiasa barani Afrika kushirikiana.
Alisema badala ya kuuchukulia upinzani kuwa adui, wanafaa kuchukuliwa kuwa washirika katika kuimarisha demokrasia inayoheshimu sheria.
Kufuatia taarifa hiyo mchanganuzi wa maswala ya kisiasa kutoka chuo kikuu cha kikatholiki cha Ruaha Prof Gaudence Mpangala alinukuliwa na gazeti la The Citizen nchini Tanzania akisema kuwa taarifa hiyo ya rais Kikwete inafaa kupongezwa.
Bwana Mpangala amesema kuwa ni muhimu kwamba taarifa hiyo inatoka kwa kiongozi mwandamizi katika chama cha CCM.
''Tunaunga mkono taarifa ya Kikwete. Kuna tatizo kubwa na tunahitaji kutafuta suluhu ya kukabiliana nalo, Bwana Mpangala alinukuliwa na gazeti la The Citizen nchini Tanzania akisema.
Akiongezea: Kuendelea kuwanyima wapinzani haki ya kutekeleza wajibu wao ni sawa na kuwanyima raia haki zao kimaendeleo.
Kwa mujibu wa gazeti hilo bwana Mpangala amesema kuwa matatizo mengi yanayokabili Afrika yanatokana na ukandamizaji wa sera za kidemokrasia.
Vilevile mwalimu wa chuo kikuu cha Dar es Salaam Richard Mbunda amesema kuwa ushauri wa rais Kikwete unaonyesha kitu ambacho alikuwa akifanya katika uongozi wake wa miaka 10 nchini Tanzania.
Akizungumza na The Citizen alisema: Tumefanikiwa pakubwa katika kukuza demokrasia na kuheshimu sheria katika miaka ya nyuma lakini sasa tunarudi nyuma.
''Ni lazima turudi katika mwelelekeo unaofaa'', alisema akiongezea :hii tabia ya watawala kuwachukulia wapinzani kama maadui inaufanya upinzani kuitazama serikali kama aduia wake''.
Naye mshirikishi wa muungano wa watetezi wa haki za kibinaadamu THRDC bwana Onesmus Ole Ngurumwa amesema kuwa taarifa ya rais Kikwete ni funzo kubwa kwa wanasiasa barani Afrika na husuaan Tanzania.
Amewataka viongozi wa zamani kujitokeza hadharani na kuliangazia tatizo hilo huku akiwashauri wapinzani kutoogopa kufanya mazungumzo na rais Magufuli ili kutafiut suluhu ya kudumu.
''Kenya ni mfano mzuri kwetu katika eneo hili.Upinzani unatumia uhuru wa kidemokrasia na imesaidia kundoa hali ya wasiwasi mbali na kuimarisha maenedeleo''.alisema.