WANAFUNZI watatu waliopata ajali ya basi la Shule la Lucky Vincent ya jijini Arusha Mei mwaka huu katika eneo la Rhotia wilayani Karatu, wamehudhuria masomo yao darasani jana kwa mara nyingine huku wanafunzi wenzao wakifurahi.

Wanafunzi hao Sadya Awadhi, Wilson Tarimo na Doreen Elibariki, waliwasili kwa usafiri wa pamoja binafsi shuleni eneo la Kwa Mrombo huku wakisindikizwa na wazazi wao. Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Lucky Vincent, Longino Mkama, watoto hao waliwasili jana asubuhi, na walipofika walipokelewa na wanafunzi wenzao huku kila mmoja akishangilia hususan wanafunzi wa darasa la saba, waliokuwa wakisoma nao kabla ya kupata ajali iliyosababisha wapelekwe Marekani kwa matibabu zaidi.
“Ukweli tumejisikia faraja kuwaona watoto hawa wakiwa darasani wakihudhuria masomo yao na wenzao na hawaoneshi tofauti yoyote na sisi tumewapokea na wanaendelea na masomo yao hadi watakapofanya mitihani yao,” alieleza Mwalimu Mkama.
Mama mzazi wa Wilson, Neema Temba alisema amefurahi kuwaona watoto wao wakienda shule ikiwemo mapokezi kwa wanafunzi wenzao. Akizungumzia kuhusu watoto hao kutumia usafiri wa mabasi ya shule, alisema hawatatumia mabasi ya shule kwa kuwa bado wana hofu na ajali, hivyo wazazi wao kwa pamoja wameamua kutumia usafiri wa magari binafsi kuwapeleka shuleni asubuhi kisha kuwarudisha majumbani mwao nyakati za jioni.
“Hatujawaruhusu kutumia usafiri wa shule, wana hofu nao sana hivyo tutawapeleka kwa magari yetu binafsi asubuhi na jioni kuwarudisha majumbani hadi hapo watakapomaliza mitihani yao,” alieleza Temba.
Juzi wazazi wa watoto hao walimuomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kuwasaidia ili watoto wafanye mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka huu. Aidha, Gambo alikabidhi Sh 23,273,885 kwa wazazi watatu ambapo kila familia ilipewa Sh mil. saba.