MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amefi chua uovu wa kutisha unaofanywa na askari polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam na kuagiza Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuwakamata askari waliojihusisha na uovu huo na kuwafungulia mashitaka mara moja.

Makonda alisema askari polisi hao wamekuwa wakifanya kazi zao kinyume na maadili, ikiwemo kujihusisha na kuchukua fedha za watuwanaokamatwa na dawa za kulevya. Makonda alitoa kauli hiyo jana wakati akipokea msaada wa pikipiki 10 zenye thamani ya Sh milioni 40 zilizotolewa na kampuni ya kichina ya Tongbar, kwa ajili ya Kikosi cha Usalama Barabarani.
Alisema, katika tukio la kwanza, polisi mkoani humo walipata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba kuna mfanyabiashara mkubwa wa dawa za kulevya alikuwa amefikia katika hoteli moja ya kifahari ambayo hakuitaja. Alisema baada ya polisi hao kupata taarifa hizo walifika katika hoteli hiyo na kumkamata mtuhumiwa kisha kuondoka naye lakini hawakumfikisha kituoni badala yake walimpeleka walikokujua wao na kupewa rushwa kisha wakamuachia.
Alisema baada ya mtuhumiwa huyo kuachiwa alirudi hotelini na kuanza kuwafanyia fujo wafanyakazi wa hoteli hiyo ili wamtaje aliyetoa taarifa polisi dhidi yake. “Hii ni ajabu sana, alifanya fujo baada ya kuona hivyo wenye hoteli wakatoa tena taarifa polisi. Tulipokwenda kwenye ile hoteli na kuangalia kwenye kamera za CCTV tuliona wale askari wakiingia mle ndani na kumchukua yule mtu na matokeo yake hawajulikani walimpeleka wapi,” aliongeza Makonda.
Aidha alisema anazo taarifa za polisi waliomkamata mtu na mpenzi wake na kuwapiga picha za utupu wakiwa katika gari na kuwabambikizia kesi kwamba walikuwa wakifanya mapenzi, kisha kuomba rushwa ya Sh milioni tano ili wasitoe picha zao hadharani. Pia alisema kuna askari wengine wamekuwa wakiwakamata watu katika ufukwe wa Coco kisha kuwabambikizia kesi kwamba wamekutwa wakifanya mapenzi hadharani.
Makonda pia alibainisha kuwa kuna askari wa kituo cha polisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), walivamia nyumba ya raia kwa kisingizio kuwa wanapekua dawa za kulevya na kuchukua kitita cha dola 50,000 za Marekani. Pia alisema ana taarifa za baadhi ya askari wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kushirikiana na raia wa China, kupitisha kwa siri viumbe hai ambavyo ni maliasili ya taifa.
Kufuatia kauli hiyo Makonda alimpa saa nne Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kuwatia mbaroni askari hao na kuwafunguliwa mashitaka kwa mujibu wa sheria. “Ifikapo saa 10 alasiri (jana) nipate taarifa kwamba polisi hawa wote wawe wametiwa ndani, kuanzia wale waliofanya tukio la hotelini Kinondoni, uwanja wa ndege na sehemu nyingine.
Washitakiwe kwa mujibu wa sheria za Jeshi la Polisi,”alisema. Alisema matukio hayo ya baadhi ya polisi yanatoa taswira kwamba hawawajibiki kikamilifu kuwalinda raia na mali zao na wanahatarisha usalama wa wananchi kwa kuruhusu wauza unga waendelee kuwepo mtaani. “Nataka nitume salamu kwa Jeshi la Polisi, hakuna mtu atakayeendelea kutumia magwanda na sheria ya kuwa polisi kwa ajili ya kuwakandamiza wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Tupo kwa ajili ya kusimamia sheria, tupo kwa ajili ya kuwalinda wananchi na mali zao na tupo kwa ajili ya kushughulika na wahalifu. Haiwezekani waturudishe nyuma,” alionya Makonda. Akizungumzia utekelezaji wa agizo hilo la kuwakamata askari husika kabla ya saa 10 jioni jana, aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ambaye amehamishiwa mkoani Mtwara, Lucas Mkondya alisema Polisi ilikuwa inawasiliana na Mkuu huyo wa Mkoa ili kupata orodha kamili ya askari waliohusika na matukio hayo na kwamba kazi ya kuwakamata ingeanza wakati wowote jana na leo.