Afisa wa cheo cha juu wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya IEBC, ambaye alitoweka siku ya Ijumaa usiku, amepatikana akiwa amefariki.
Mwili wa Christopher Chege Msando, ambaye alikuwa kaimu mkurugenzi wa masuala ya teknolojia wa IEBC, umepatikana kwenye chumba kimoja cha kuhifadhia maiti jijini Nairobi.

Mawasiliano ya mwisho kutoka mwa Musando aliyafanya siku ya Jumamosi mwendo wa saa tisa alifajiri kupitia ujumbe wa SMS kwa mmoja wa wafanyakazi wenzake.
"Hakuna shaka kwamba aliteswa na kuuawa," mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati ameambia wanahabari.
"Swali pekee lililo katika akili zetu ni kuhusu nani alimuua na ni kwa nini aliuawa siku chache hivi kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika," shirika la habari la AFP limemnukuu Bw Chebukati akisema.
Kisa hiki kinatokea ikiwa imesalia juma moja kabla ya kuandaliwa uchaguzi mkuu nchini Kenya ambao utafanyika tarehe 8 Agosti.
Polisi wanasema kuwa mwili wa afisa huyo pamoja na wa mwanamke ambaye hakutambuliwa, ilipatikana eneo la Kikuyu lililo viungani mwa mji wa Nairobi na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City Mortuary.
Mkurugenzi mkuu wa IEBC Ezra Chiloba (kushoto) akiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City
Image captionMkurugenzi mkuu wa IEBC Ezra Chiloba (kushoto) akiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City
Bw Msando alikuwa akihusika na usambazaji wa vifaa vya eletroniki ambavyo vingetumiwa kutambua wapiga kura na kwa upeperushaji wa matokeo wakati wa uchaguzi mkuu wiki ijayo.
Taarifa zinasema kuwa mwili wa Musando ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City Jumamosi asubuhi na watu waliojitambulisha kuwa maafisa wa polisi.
Afisa mkuu mtendaji wa tume hiyo Ezra Chiloba alikuwa miongoni mwa maafisa wakuu wa IEBC waliofika katika ufuo huo kutoa rambirambi kwa jamaa na marafiki wa marehemu waliofika kuuona mwili.
Mwili wa Bw Msando umesafirishwa hadi chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee Funeral Home.
Mwili wa Musando ukiwekwa kwenye gari kupelekwa Lee Funeral Home
Image captionMwili wa Musando ukiwekwa kwenye gari kupelekwa Lee Funeral Home

Msando alikuwa nani hasa?

Bw Musando alikuwa mtaalam wa maswala ya teknolojia, na alikuwa amefanya kazi katika mashirika makubwa nchini kenya.
Alikuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa idara ya teknolojia ya IEBC, baada ya aliyekuwa mkurugenzi mkuu kuachishwa kazi kwa muda kwa madai ya kupinga zoezi la kupiga msasa mitambo ya teknoljia ya IEBC.
Bw Musando alikuwa akizungumza kwa uwazi kwenye vyombo vya habari kuhusu mikakati ambayo tume hiyo imeweka ya kuhakikisha kwamba utambuzi wa wapiga kura kiteknolojia na usambazaji wa matokeo ya kura unafanikishwa bila vikwazo vyovyote.
Shinikizo kwa IEBC
Kifo cha musando kinajiri wiki moja tu kabla ya uchaguzi ulio na ushindani mkubwa kufanyika.
Tume ya uchaguzi imekuwa chini ya shinikizo kali za kufanikisha uchaguzi huru na na ulio uwazi. Tume hiyo imewekeza katika teknolojia ya kisasa japo Wakenya na vyama vya kisiasa wamekuwa wakitilia shaka uwezo wa tume hiyo wa kufanikisha uchaguzi huru.
Uchaguzi wa mwaka huu una ushindani mkubwa baina ya rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake wa muda mrefu Raila Odinga.
Uchaguzi wa mwaka huu umegubikwa na wingu la shutuma na lalama hususan kutoka kwa upinzani, ambao unadai kwamba serikali ina mpango wa kutumia wanajeshi kuiba kura, huku tume ya uchaguzi ikilaumiwa kwamba imekiuka sheria kwa kuchapisha makaratasi zaidi ya kupiga kura.