Michuano ya soka ya “Ikungi Elimu Cup 2017” imezinduliwa kwa kishindo katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida baada ya mamia ya wakazi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo.
Michuano hiyo iliyoandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi na kuendeshwa na Chama cha Soka wilayani Ikungi, ilizinduliwa jumamosi Agosti 19,2017 katika uwanja wa shule ya sekondari Ikungi huku ikitarajiwa
kushirikisha timu 69 wilayani humo.
Mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala mkoa wa Singida Dkt.Angeline Lutambi, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida ambaye alipongeza wazo la kuanzishwa kwa michuano hiyo inayolenga kuhamasisha wananchi pamoja wadau mbalimbali ndani na nje ya wilaya ya Ikungi ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kutatua changamoto za elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa, maabara, vyoo pamoja na nyumba za waalimu.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mhe.Miraji Mtaturu ambaye ni mlezi wa mfuko wa elimu Ikungi, alisema michuano hiyo itasaidia upatikanaji wa shilingi bilioni tatu kupitia mfuko wa elimu Ikungi katika kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya kusaidia utatuzi wa kero za elimu wilayani huo.
Uzinduzi wa michuano hiyo, ulikwenda sambamba na uzinduzi wa zoezi la ufyatuaji wa matofali kwa ajili ya ujenzi wa maabara uliokwama tangu mwaka 2009 katika shule ya sekondari Ikungi hii ikiwa ni uzinduzi rasmi wa zoezi kama hilo kwenye kata zote wilayani Ikungi ambapo kila Kata imepewa jukumu la kufyatua matofali elfu kumi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na nyumba za waalimu.
Katika zoezi hilo, walijitokeza wadau pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani, wenyeviti wa halmashauri, jeshi la polisi, Tanesco na wanachi ambao walimuunga mkono Mkuu wa wilaya ya Ikungi, Mhe.Mtaturu aliyekabidhi mifuko 100 ya simenti na wao wakachangia fedha taslimu zaidi ya shilingi 800,000 na ahadi zaidi ya shilingi 1,900,000, ahadi za simenti mifuko 194 na mchanga wa moramu malori matano kutoka kwa mdau wa maendeleo wilayani Ikungi Hussein Sungita.
Aidha mgeni rasmi aliwakabidhi shilingi laki moja kila mmoja, jumla ya wanafunzi 16 wa kidato cha sita shule ya sekondari Ikungi waliopata daraja la kwanza kwenye mtihani wao ikiwa ni ahadi ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu aliyoitoa wakati wa mahafali ya wanafunzi hao huku akiwaahidi walimu shilingi milioni moja kwa kila wanafunzi 10 wenye madaraja ya kwanza.
Nazo timu 69 zinazoshiriki michuano hiyo ya “Ikungi Elimu Cup 2017” zilipokea vifaa vya michezo ikiwemo jezi na mipira kwa ajili ya michuano hiyo ambapo jana zilipigwa mechi mbili za kirafiki, ya kwanza ikiwa ni kati ya madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Singida dhidi ya madiwani wa halmashauri ya Ikungi ambapo mchezo huo ulimalizika kwa sare tasa.
Mchezo wa pili ulikuwa kati ya Ikungi United dhidi ya Puma ukimalizika kwa puma kuwashangaza Ikungi waliokuwa wanaongoza kwa bao mbili hadi kipindi cha kwanza, baada ya kusawazisha na kujipatia bao la ushindi katika kipindi cha pili na hivyo matokeo kuwa Puma 3-2 Ikungi.
0 Comments