Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lucas Mkondya
JESHI la Polisi limesema linafanya uchunguzi kuhakikisha linawatia mbaroni watu waliompiga risasi na kumuua Mkurugenzi na Mwanzilishi-Mwenza wa Shirika lisilo la kiserikali la PAMS Foundation, Wayne Lotter jijini Dar es Salaam juzi.
Lotter ndiye aliyefanikisha kukamatwa kwa mfanyabiashara kinara wa meno ya tembo, Yang Feng Glan maarufu kama ‘Malkia wa Meno ya Tembo’ hivi karibuni baada ya mhalifu huyo kusakwa kwa muda mrefu katika mataifa mbalimbali duniani.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema linafanya upepelezi wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa linawatia mbaroni wahusika wa mauaji hayo huku Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe akieleza kusikitishwa na tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Kamanda Kanda Maalumu, Lucas Mkondya alisema tukio hilo lilitokea Agosti 16, saa tano maeneo ya makutano ya barabara ya Haile Selassie na Kaole eneo la Masaki.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema Lotter (51), alipigwa risasi katika maeneo hayo ya Masaki, wakati akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ambapo teksi aliyopanda ilisimamishwa na gari lingine kabla ya watu wawili kutelemka na kumpiga risasi.
Lotter alikuwa Mkurugenzi na Mwanzilishi-Mwenza wa PAMS Foundation, Shirika lisilo la Kiserikali ambalo linajihusisha na masuala ya kupinga ujangili ambalo lilianza shughuli zake Tanzania mwaka 2009.
Imeelezwa kuwa Lotter amekufa huku akiwa amepanga kufanya mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ujangili wa tembo ikiwemo kuzindua vilabu vya kupinga ujangili, kufunga vifaa vya GPS kwa tembo wote nchini, pia alikuwa msaada kwa serikali kupitia miradi mbali mbali kama vile kufanikisha kumkamata malkia wa ndovu aliyekuwa anatafutwa Dunia nzima ambaye alikamatwa nchini miezi michache iliyopita.
Pia alianzisha vikosi vya ulinzi (game rangers) ambao aliwalipa ili kusaidia ulinzi wa tembo kwenye mbuga mbalimbali nchini. Alifadhili pia filamu ya The Ivory Game iliyochezewa Tanzania na China, ambayo ilizinduliwa Hollywood, Marekani ikionesha ujangili unavyofanyika na pia alisaidia magari ya doria kwa Jeshi la Polisi na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Polisi waanza uchunguzi Kamanda Mkondya alisema wauaji hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi mbali na kumuua mkuregenzi huyo, walipora kompyuta mpakato tatu, simu moja aina ya Nokia na nyaraka mbalimbali Alisema marehemu alikuwa akitokea mkoani Arusha akiwa amepanda gari ya kukodi yenye namba za usajili T 499 DEV aina ya Toyota Sienta pamoja na mfanyakazi mwenzake, Christine Clarkl (40) raia wa Afrika Kusini.
Mkondya alisema raia hao walikuwa wanaelekea Bawbaw Apartment zilizoko maeneo ya barabara ya mwaya Masaki kwa ajili ya mapumziko ambapo wakiwa njiani alitokea mtu mmoja akiwa na gari na kuwaziba kwa mbele akiwa amevaa koti jeusi na baadaye alifyatua risasi mbili akidai apewe dola ambapo risasi ilimjeruhi marehemu mdomoni na baadaye alifariki dunia akiwa anapelekwa Hospitali ya Sami iliyopo Masaki kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Waziri Maghembe amlilia Akizungumzia mauaji hayo, Waziri Maghembe alieleza kusikitishwa na kifo hicho kwa kusema mkurugenzi huyo alikuwa mshirika mkubwa wa kupambana na ujangili.
‘’Hatujui aliyefanya mauaji haya, lakini tumeiachia Polisi kufanya uchunguzi ambapo nimepata taarifa kuwa mwelekeo wa uchunguzi unakwenda vizuri, hivyo tunasubiri taarifa ya Polisi ndipo tutazungumza mambo mengi,’’ alisema.
Meno ya tembo 28 yanaswa Dar Katika tukio jingine, watu sita akiwemo Imam wa Msikiti wa Huda uliopo Mbezi Beach Dar es Salaam, Bakari Seruni wamekamatwa na meno ya tembo 28, tembo wanaodhaniwa kuuawa kati ya mwaka 2013 na 2014.
Mbali na Seruni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Beach, watuhumiwa wengine ni Mohamed Mohamed maarufu kama Mpemba, Juma Jebo mkazi wa Manzese, Hamis Omary, Amir Shelukindo mkazi wa Gairo Morogoro na Ahmed Bakari mkazi wa Mkuranga.
Waziri Maghembe alisema kuwa meno hayo yalikamatwa kati ya Agosti 13 na 14, mwaka huu ambapo yalikuwa yamehifadhiwa kwenye ghala lililopo Mbezi Beach yakisubiri kupelekwa sokoni.
Profesa Maghembe aliongeza kuwa walikamata vipande 21 vyenye uzito wa kilogramu 310.2 na kwamba kati ya watuhumiwa hao, mmoja wapo aliwasihi wasimkamate mke wake kwa kuwa ana meno ya tembo vipande saba vyenye uzito wa kilogramu 66.8.
‘’Serikali inafanya kazi ya kuwatafuta na kuwapata majangili wote na watakiona cha mtema kuni kwani wanafanya juhudi za kumaliza urithi wa wanyamapori kwa watoto wetu,’ ’alisema Profesa Maghembe.
Pia alisema watu wanaofikiri kuwa biashara hiyo ina faida watafute kazi nyingine ya kufanya na washiriki katika kuhifadhi maliasili za taifa. Alifafanua kuwa kumekuwa na biashara ya meno ya tembo kupitia mitandao hivyo jitihada za kupambana na majangili zinaendelea kwani hata idadi ya wanyama wanaouawa imepungua.
‘’Tutazungumza na Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya kudhibiti biashara hii kwa nchi nyingine ambazo zinaruhusu kama vile Vietnam na Thailand ili kuzuia mianya yote ya biashara ya meno ya tembo kuuzika duniani,’’ alisisitiza. Imeandikwa na Sophia Mwambe na Francisca Emmanuel Dar.