Mwamuzi maarufu katika mchezo wa kandanda nchini Somalia amepigwa risasi na kuuawa karibu na nyumbani kwake mjini Mogadishu.
Osman Jama Dirah, ambaye alisimamia mechi za kanda na kimataifa, aliuawa akiondoka msikitini kurejea kwake nyumbani katika mtaa wa Wardhigley.
Taarifa zinasema wanaume wawili waliokuwa na bastola walimfatulia risasi mara kadha.

Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Somalia Anas Ali Mohamud amenukuliwa akisema aliwaona washambuliaji wakiondoka eneo la mauaji.
Anasema maafisa wa usalama walifika eneo hilo baadaye lakini kufikia sasa hawajafanikiwa kuwakamata wahusika.
Mwandishi wa BBC Somali Ahmed Adan anasema kuuawa kwa Osman Jama Dirah ni pigo kubwa sio tu kwa tasnia ya soka nchini Somalia bali kwa sekta yote ya michezo nchini humo.
Alikuwa miongoni mwa marefa maarufu zaidi nchini humo tangu kusambaratika kwa serikali kuu miaka 27 iliyopita.
Dirah alifahamika kama mwamuzi bora zaidi na alihudumu katika kamati ya waamuzi katika Shirikisho la Soka la Somalia.
Alisimamia mechi za kanda na kimataifa na alihduumu kama mwamuzi kwa zaidi ya miaka 25.
Alianza kushiriki katika kandanda mwaka 1979, kama mlinda lango wa timu ya Galgadud, na baadaye akajiunga na timu ya taifa kama mlinda lango.
Mwaka 1997, aliteuliwa kuwa mwamuzi na FIFA nchini Somalia.
Sababu ya kuuawa kwake bado haijabainika, na kufikia sasa hakuna aliyedai kuhusika.
Kuuawa kwa watu mashuhuri hata hivyo si jambo geni lakini haijulikani ni kwanini afisa wa soka alilengwa.
Mwili wa Dirah utazikwa baadaye leo mjini Mogadishu.