Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Makamu wa Raisi wa Kampuni
(Uendelezaji Bibiashara) wa Kampuni ya PIRIOU ya utengenezaji na
ukarabati wa meli nchini Ufaransa. Bwana Michel Perrin .kulia ni Balozi
wa Tanzania Nchini Ufaransa Bwana Samweli Shelukindo.Waziri Mkuu
amekutana naye leo Agost 29/2017 Parisi Ufaransa.Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu.
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka watu wote wenye nia ya kutaka kuwekeza
katika miradi mbalimbali nchini Tanzania kuhakikisha wanafuata sheria,
kanuni na taratibu.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Agosti 29,
2017) wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais
(Uendelezaji Bishara) wa kampuni ya PIRIOU, Bw. Michel Perrin. Waziri
Mkuu amekutana na Bw. Perrin jijini Paris nchini Ufaransa kupitia ofisi
ya ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa. Kampuni ya PIRIOU inataka kuja
nchini kuwekeza katika utengenezaji na ukarabati wa meli.

Akizungumza
na muwekezaji huyo Waziri Mkuu alimshukuru kwa nia yake ya kutaka
kuwekeza nchini, ambapo alimtaka afuate sheria, kanuni na taratibu za
uwekezaji nchini. “Tanzania ni sehemu nzuri ya uwekezaji kwa sababu kuna
fursa nyingi. Pia ni nchi yenye amani na utulivu wa kisiasa pamoja na
mazingira mazuri ya uwekezaji hivyo nakukaribisha sana.”

Kwa
upande wake Bw. Perrin amesema ameamua kuja kuwekeza nchini kwa kuwa
Tanzania ni nchi salama na kwamba anauhakika wa kupata soko ndani ya
nchi pamoja na mataifa jiraji. Amesema anaamini uwekezaji wake nchini
Tanzania utakuwa na tija, hivyo ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano wa
karibu na Serikali na pia atahakikisha anafuata sheria zote za nchi.

Pia
Bw. Perrin alitumia fursa hiyo kumshukuru Balozi wa Tanzania nchini
Ufaransa, Balozi Samwel Shelukindo kutokana na ushirikiano anaompa
kuhusu masuala ya uwekezaji nchini. Naye Balozi Shelukindo amesema
atahakikisha anaendelea kutafuta wafanyabiashara mbalimbali na
kuwashawishi waje kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU, JUMANNE, AGOSTI 29, 2017.