Wapiganaji wa kundi la Kiislamu al-Shabab wameshambulia kambi ya jeshi na kituo cha polisi nchini Somalia karibu na mpaka wa nchi hiyo na Kenya, afisa wa serikali amesema.
Kundi hilo la al-shabab lilivamia kambi iliyoko katika mji wa Beled Hawa kwanza kwa kuvurumisha gari lililokuwa limejazwa vilipuzi na kisha wanamgambo hao wakaingia na kushambulia wakitembea kwa miguu, afisa huyo wa serikali Mohamud Hayd amesema.

Al- Shabab wamesema wamewaua wanajeshi 30 katika shambulio hilo ambalo walilitekeleza na kisha kutoroka.
Al-Shabab wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara nchini Somalia na Kenya tangu kuanzishwa kwa kundi hilo la wanamgambo lililobuniwa zaidi ya muongo mmoja uliopita.
Umoja wa Afrika (AU) una karibu kikosi cha wanajeshi 18,000 wanaosaidiwa serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kukabiliana na wanamgambo hao.
Shambulizi hilo katika eneo la Beled Hawa, pia liliwaacha wakazi wengi na majeraha.
Wanamgambo hao pia waliteketeza moto kituo cha polisi na mnara wa mawasiliano kabla ya kutoweka Bw Osman aliongeza.
Shambulizi hilo limedhihirisha al-Shabab bado ni hatari, licha ya kupoteza maeneo mengi waliyoyadhibiti awali kwa wanajeshi wa Muungano wa Afrika na hata makomanda wao wakuu kuuawa katika mashambulio la ndege za Marekani, ripoti kutoka kwa mwandishi wa BBC Idhaa ya Kisomali Bashkas Jugsodaay kutoka jijini Nairobi.
Mwezi Januari al-Shabab walisema wamewaua wanajeshi 50 kutoka Kenya katika shambulio kwenye kambi yao ya Kolbiyow iliyoko kusini mwa Somali.
Jeshi la Kenya ni miongoni mwa wanajeshi wa muungano wa Afrika wanaopigana na al-Shabab nchini Somali