Shirika la kimataifa linalotetea haki za binadamu la Amnesty International limeonya kuwa Maelfu ya wakimbizi wa Burundi wanaorudi nchini kwao kutoka Tanzania wanakabiliwa na hatari za kiusalama nchini mwao.

Mwezi uliopita, Tanzania, Burundi na shirika la umoja wa mataifa linalohudumia wakimbizi UNHCR walikubaliana kwamba kufikia mwisho wa mwaka huu wawe wamewarejesha wakimbizi elfu kumi na mbili wanaoishi Tanzania na wanataka kurudi kwao Burundi kwa hiari.
Lakini Amnesty International linasema, mpango huu unahatarisha maisha ya maelfu ya wakimbizi na linaamini kuwa wakimbizi wengi wanarejeshwa nyumbani kwao kutokana msukumo wa ushawishi kutoka serikali ya Tanzania na Burundi.
Shirika hilo limedai kuwa hali ya usalama bado sio shwari katika ripoti yao inayotoka leo, wanasema visa vya kuteswa, kufungwa bila makosa, kubakwa na hata kuuwawa bado vinaendelea.