KAMPUNI inayojishughulisha na huduma za hoteli na tiketi za ndege kwa njia ya mtandao barani Afrika, Jumia Travel imemtangaza Bw. Joe Falter (pichani) kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu mpya akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Paul Midy ambaye amechaguliwa kushika wadhifa mkubwa zaidi kwenye makampuni ya Jumia. Bw. Falter ambaye pia ni mwanzilishi na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni dada ya Jumia Food, amechukua majukumu hayo ikiwa ni jitihada za kuimarisha zaidi shughuli za uendeshaji wa kampuni hiyo.



“Nimefurahia sana kujiunga na timu mpya ya Jumia Travel ambayo imejizatiti kwenye kuleta mabadiliko ya namna watu wanavyosafiri ndani na nje ya bara la Afrika. Ikiwa na idadi ya orodha kubwa ya hoteli na kuongoza kiubunifu, bila ya shaka Jumia Travel ni kinara katika masuala ya usafiri, utalii na ukarimu, nimejawa na shauku kubwa ya kuhakikisha tunasonga mbele zaidi,” alisema Joe.

Kabla ya hapo, Joe alikuwa ni mshauri wa masuala ya usimamizi katika taasisi ya McKinsey ya jijini London nchini Uingereza, akiwa na rekodi nzuri ya kuyanyanyua makampuni ya Ulaya na Afrika, hivyo amekuja na ujuzi wa kipekee wa mikakati ya kiusimamizi ambayo itasaidia katika kukuza fursa za biashara zinazochipukia.

Akizungumzia juu ya kuteuliwa kama bosi mpya wa Jumia Travel, Joe anahakikisha kwamba, “Jumia Travel imekua kwa kiasi kikubwa ndani ya miaka miwili iliyopita na lengo kubwa ni kuendeleza jitihada hizi za ukuaji wa haraka huku tukiimarisha huduma zetu kwa wateja na hoteli tunazofanya nazo kazi. Washirika wetu wa hoteli ambao ni zaidi ya 30,000 Afrika na mamia ya maelefu ya wateja watajionea maboresho mapya kwenye njia za mtandao na za kawaida.”

“Nina ujasiri kwamba Joe ni chaguo sahihi la kiongozi ambaye ataipelekea Jumia Travel kuwa chaguo pekee kama wakala wa usafiri Afrika na nje ya mipaka,” alisema mwanzilishi mwenza wa Jumia, Sacha Poignonnec.

Ikiwa imeanzishwa mwaka 2013, Jumia Travel imejitengenezea rekodi nzuri katika masuala ya huduma za kimtandao na ubunifu wa kiteknolojia, na kuwa kinara katika makampuni ya uwakala wa usafiri barani Afrika. Inatoa huduma za hoteli na tiketi za ndege kwa njia ya mtandao pamoja na kuandaa vifurushi vya aina mbalimbali kwa ajili ya wateja wake, watu binafsi na kwa ajili ya makampuni.


Kuhusu Jumia Travel

Jumia Travel (www.travel.jumia.com) ni kampuni nambari moja barani Afrika katika utoaji wa huduma za usafiri mtandaoni, inarahisisha huduma za usafiri kwa kumpatia uzoefu mtumiaji kwa kulinganisha bei na huduma zinazopatikana kwa njia ya haraka na salama zaidi.

Ikiwa ina hoteli zaidi ya 30,000 Afrika (na zaidi ya hoteli 300,000 duniani) na makampuni ya ndege zaidi ya mia moja kama washirika wake, Jumia Travel inalenga kutoa uhuru wa kusafiri kupitia kupunguza gharama za kusafiri, kutoa orodha kubwa ya hoteli na kuwezesha huduma bora na zenye viwango vya juu kwenye kila nchi husika ili kuwa mojawapo ya sehemu ambayo mteja atakidhi haja zake zote za kiusafiri barani.

Jumia Travel inafanya shughuli zake katika nchi zaidi ya 40 za Afrika, ikiwa na ofisi kwenye nchi 10 miongoni mwake, na wataalamu wa masuala ya kusafiri zaidi ya 400 ambao wapo tayari kuwahudumia wateja wakati wowote. Ofisi zetu kuu zinapatikana Lagos (Nigeria), Accra (Ghana), Dakar (Sénégal), Abidjan (Ivory Coast), Algiers (Algeria), Douala (Cameroon), Kampala (Uganda), Dar Es Salaam (Tanzania), Nairobi (Kenya) na Addis Ababa (Ethiopia). Kabla ya mwezi Juni 2016, Jumia Travel ilikuwa ikijulikana kama Jovago.

Ilianzishwa 2013 na Jumia huku ikiendeshwa kwa ushirikiano wa MTN, Rocket Internet, Millicom, Orange, Axas na washirika wengine.