Rais wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.
RAIS Dk John Pombe Magufuli amepokea ripoti za uchunguzi wa madini ya Tanzanite na Almasi kutoka kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Ripoti hizo zimetokana na kamati mbili zilizoundwa na spika wa Bunge Job Ndugai. Mara baada ya kupokea ripoti hizo, Rais Magufuli ametengua uteuzi wa wateule wote waliotajwa katika ripoti hizo.

Miongoni mwa wateule wa Rais waliotajwa katika ripoti hiyo ni pamoja na Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, George Simbachawene, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Edwin Ngonyani. Wengine waliotajwa katika taarifa hizo ni pamoja na Katibu Tawala Eliakim maswi, wabunge Willium Ngeeleja na Endrew Chenge.
"Kuna baadhi ya wabunge kama ulivyosema mheshimiwa Spika, kila mahali yupo, katika kashfa fulani yupo, katika hili yupo, katika lile yupo. Tena wengine bado wapo bungeni na wakati mwingine wanachangia mpaka mishipa inawatoka, taratibu zifanyike kuwachukulia hatua" Rais Magufuli Rais Magufuli amewasifu watanzania wazalendo ambao wako tayari kutoa uhai wao kwa ajili ya Taifa lao.
"Tunawatumia watanzania wazalendo kupata taarifa za kizalendo kwa Taifa letu, wapo watanzania wanaorubuniwa na kuisaliti nchi yao, hao hawafai" Rais Dk John Pombe Magufuli, Ikulu. Dar es Salaam.
Katika maelezo yake kabla ya kumkabidhi Rais ripoti hizo, Majaliwa amesema kwa muda mrefu watanzania wamekuwa wakilalamika serikali kutowajali na kuwasikiliza. Amesema kupitia serikali ya Awamu ya Tano sasa watanzania wote watakuwa na haki sawa na wote watasikilizwa.
"Watanzania ambao kwa miaka mingi wamejihisi hawasikilizwi na hawahurumiwi sasa ni wakati wao kujihisi kuwa ni watanzania na wanastahili haki zote kama watanzania kupitia serikali yako mheshimiwa Rais" Kassim Majaliwa
Rais Magufuli amemkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kwa ripoti hizo za madini kwa ajili ya kufanyiwa kazi mara moja.