WABUNGE wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, leo wamegoma kuhudhuria kuapishwa kwa Wabunge wapya wa viti maalum kutoka Chama cha wananchi CUF, kazi iliyofanyika Bungeni na kuongozwa na Spika wa Bunge Job Ndugai.
Wakiwa wamevalia nguo nyeusi wabunge hao kutoka vyama vyote vya upinzani bungeni hata wale wa CUF walikuwa katika makundi nje ya Ukumbi wa Bunge katika jengo la zamani la Ukumbi wa Pius Msekwa.

Baadae baada ya kukamilika uapishaji wa wabunge wapya ndani ya ukumbi wa Bunge, waliandamana kwa pamoja hadi katika lango kuu la Bunge na kukusanyika kasha kuzungumza na waandishi wa habari juu ya uamuzi wao huo wa kugomea shughuli ya kuapisha Wabunge wapya wa kambi hiyo Bungeni.
Katibu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambaye pia ni Mbunge wa Momba, kupitia Chama cha Demorasia na Maendeleo Chadema, David Silinde alizungumza na wanahabari na kusema kuwa wamefanya hivyo kuunga mkono wenzao waliofukuzwa na kufungua kesi Mahakamani.


Silinde alisema hawatawaunga mkono wala kushirikiana na wabunge hao wapya wa CUF hadi Kesi ya Msingi iliyopo Mahakamani itakapo kamilika. “Tumefanya hivi na tutaendelea na msimamo wetu wa kutoshirikiana na wabunge hawa hadi pale kesi ya Msingi itakapoisha Mahakamani,” amesema Silinde.