Watu 35 wameripotiwa kuuawa katika jimbo la Kati la Plateau kufuatia shambulio lililofanywa na watu wenye silaha katika vijiji kadhaa.
Mashambulizi hayo yamefanywa katika eneo la Bassa kaskazini mwa Jos, mji mkuu wa jimbo hilo. Huku amri ya kutotembea ovyo usiku ikiwekwa katika eneo hilo, kudhibiti usalama.

Jimbo hilo la Plateau katika siku zilizopita pia lilishuhudia muaaji ya kikabila na ya kidini yaliyosababisha vifo vya maelfu ya watu.
Ripoti kutoka eneo la tukio zinasema watu wenye silaha walivamia vijiji na kuanza kushambulia raia na pia kuchoma moto nyumba zao.
Viongozi wa maeneo hayo wameiambia BBC kwamba watu 29 wakiwemo wanawake na watoto walikufa, papo hapo na wengine sita walifariki siku iliyofuatia.
Polisi katika jimbo hilo la Plateau wamethibitisha shambulio hilo lakini bado hawajatoa idadi ya waliojeruhiwa.
Wanavijiji katika maeneo hayo wanawalaumu wafugaji kwa kufanya shambulio hilo, huku baadhi ya taarifa zikisema kuwa shambulio hilo ni la kulipiza kisasi kwa wafugaji hao.
Vikosi vya ulinzi vimeimarishwa zaidi katika eneo hilo, huku amri ya kutotembea usiku ikiwekwa.