Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Kenya Wafula Chebukati amewashutumu wanasiasa nchini humo akisema wanatatiza maandalizi ya uchaguzi wa marudio Alhamisi wiki ijayo.
Bw Chebukati amesema maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vyema lakini katika mazingira ya sasa ni vigumu kuandaa uchaguzi huru na wa haki iwapo hakutakuwa na mabadiliko.

Mwenyekiti huyo, ameeleza kuwa amejaribu kutekeleza mageuzi mengi kwenye maandalizi ya uchaguzi wa marudio lakini "majaribio yangu yamepingwa (kwa kura) na makamishna wengi."
"Chini ya mazingira haya, ni vigumu kuhakikisha uchaguzi huru na wa kuaminika. Nina uhakika kwamba bila mabadiliko muhimu katika sekretariati huenda tusiwe na uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika," amesema.
"Ninawahimiza wafanyakazi wa tume ambao wametajwa sana (kuhusiana na kasoro za awali) waondoke kwenye nyadhifa zao na kutoa nafasi kwa kundi maalum la kusimamia uchaguzi kufanya kazi bila kuingiliwa."
Bw Chebukati amesema hayo saa chache baada ya mmoja wa makamishna wa wa tume hiyo Dkt Roselyn Akombe kutangaza kujiuzulu akiwa Marekani na kusema hana mipango yoyote ya kurejea Kenya hivi karibuni.
Kiongozi huyo wa tume amesema mashauriano ya kisiasa yanahitajika sana kwa sasa na kutoa wito kwa viongozi wa muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) na chama cha Jubilee kukubali kulegeza misimamo yao na kushauriana.
Akombe
Ameahidi kuongoza mashauriano hayo iwapo mirengo hiyo miwili ya kisiasa itakubali kushiriki.
"Wakati umefika kwa wagombea kuacha "siasa za mgawanyiko na kuanza kuweka maslahi ya Kenya mbele ya maslahi yao binafsi."

Atajiuzulu?

Bw Chebukati amesema kujiuzulu ingekuwa hatua rahisi sana kufanya lakini kwa sasa amekusudia kuendelea kufanya kazi yake.
"Najua kuna watu wengi ambao wangefurahi zaidi kusikia nikitangaza kujiuzulu wakati huu. Kihalisia, ndilo jambo rahisi kjufanya lakini sote sharti tuweke Kenya kwanza na ndio sababu nimejitolea kuhakikisha Tume hii inafanya kazi."

Wakuu wa IEBC

Mwenyekiti: Wafula Chebukati
Naibu Mwenyekiti: Consolata Nkatha Maina
Makamishna:
  • Boya Molu
  • Paul Kibiwott Kurgat
  • Abdi Guliye
  • Margaret Wanjala Mwachanya
Afisa Mkuu Mtendaji/Katibu: Ezra Chiloba

Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC ilimtangaza Rais Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, akiwa mbele ya mpinzani wake Raila Odinga wa muungano wa upinzani Nasa kwa zaidi ya kura 1.4 milioni.
Bw Odinga alipinga matokeo hayo mahakamani na Mahakama Kuu ikaamua ulijaa kasoro nyingi na kuagiza uchaguzi mpya ufanyike katika kipindi cha siku sitini.
Tume ya uchaguzi ilitangaza tarehe mpya ya uchaguzi kuwa 26 Oktoba lakini Bw Odinga alijiondoa wiki iliyopita akisema mageuzi ambayo yalifaa kutekelezwa kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki hayajatekelezwa.