Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufaa, Semistocles Kaijage
MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, amewataka wasimamizi wa uchaguzi mdogo wa madiwani, kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ili kuepuka kuisababishia serikali hasara.
Jaji Kaijage alisema hayo mjini Dodoma jana wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi. “Tusipozingatia na kufuata taratibu za uchaguzi tunaweza kusababisha kesi nyingi za uchaguzi na kuitumbukiza nchi katika gharama ambazo zingeweza kutumika katika huduma za jamii,” alionya Jaji Kaijage.

Mwenyekiti huyo alisema kwamba hamasa katika siasa za Tanzania imeongezeka na kwamba kumekuwa na ongezeko la hali ya kutokuaminiana hasa katika mchakato wa uchaguzi na kwamba endapo wasimamizi hawatafanya kazi yao kwa ufasaha wataitumbukiza nchi kwenye matatizo makubwa.
“Mmeaminiwa na kuteuliwa kwa sababu mna uwezo wa kufanya kazi hii, kitu cha muhimu ni kujiamini na kujitambua. Pia kuhakikisha mnayajua vyema maeneo yenu mnayofanyia kazi, kuhakikisha mnawatumia vizuri wasaidizi mlio nao kwa matokeo bora,” alisema.
Jaji Kaijage aliwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo juu ya jukumu lao la kuimarisha imani ya wananchi kwa NEC, na kwamba imani hiyo itadumishwa endapo watafanya kazi kwa uwazi, uhuru na kwa ufanisi wa hali ya juu bila kuegemea upande wowote.
Aliongeza kusema kwamba uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kisheria na kikanuni zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa. “Hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na usio na malalamiko au vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi kuanzia utoaji wa fomu, uteuzi wa wagombea, uratibu wa kampeni, upigaji kura, kuhesabu kura, kujumlisha hesabu za kura na kutangaza matokeo,” alisema.
Aidha, Jaji Kaijage aliwaasa wasimamizi wenye uzoefu kujiepusha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wazingatie mafunzo ambayo watapewa na tume pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria zinazosimamia uchaguzi.
Mkutano huo wa ufunguzi ulihudhuriwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima na maofisa wa kada mbalimbali wa NEC pamoja na wasimamizi, wasimaizi wasaidizi na maafisa wa uchaguzi 230 ambao walikula kiapo cha kuheshimu maadili ya uchaguzi.
Awali Kailima alisema kwamba uchaguzi mdogo umepangwa kufanyika Novemba 26, “Uchaguzi mdogo unafanyika kwenye kata 43 ambazo zipo kwenye mikoa 19 kwenye halmashauri 36 na majimbo 37 kwa hiyo uchaguzi huu mdogo unafanyika karibia maeneo ya nchi nzima,” alisema Kailima.
Pia aliongeza kuwa uchaguzi huo unatarajiwa kuhusisha wapiga kura waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura wapatao 336,182 katika jumla ya vituo vya kupigia kura 893 ambapo kata yenye wapiga kura wengi wanafikia 58,622 na kata yenye wapiga kura wachache wanafikia 1,402.