KAMPUNI ya Tanzania, Tooku Garment Co Ltd inayotengeneza bidhaa za jeans aina ya Levism, Wrangler na The Children Place zinazouzwa nchini Marekani kupitia Mkataba wa Kutoa Fursa za Ukuaji wa Kibiashara kwa Nchi za Afrika (AGOA), imebainisha kuwa inauza kwa wingi nguo zake na kwamba bado ina soko la kutosha la bidhaa hizo.

Kampuni hiyo iliyopo chini ya Mamlaka ya Maeneo Maalumuya Uwekezaji Tanzania (EPZA) eneo la Mabibo External, Dar es Salaam, kwa sasa inazalisha jumla ya nguo za jeans 18,000 kwa siku ambazo kwa mujibu wa mahitaji, bado hazilitoshelezi soko hilo. Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kiwanda hicho katika eneo la EPZA jijini Dar es Salaam jana, Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Rigobert Massawe, alikiri kuwa kampuni hiyo inapata oda kubwa ya kusafirisha bidhaa hizo kupitia soko hilo la AGOA.
Hata hivyo, alibainisha kuwa pamoja na kupata soko hilo kubwa bado inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi na hivyo kushindwa kuzalisha kwa kiwango kinachohitajika. “Tunapata soko kubwa kupitia AGOA, hapa tulipo tayari tuna oda ya kupeleka suruali za jeans Marekani, hata hivyo, tunashindwa kukidhi mahitaji ya soko kutokana na uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi hasa eneo la uzalishaji,” alifafanua Massawe na kuongeza kuwa, wanajitahidi kukabiliana na changamoto hiyo.
Alisema asilimia kubwa ya wafanyakazi wake ni wale wenye elimu ya chini na wastani ambao inabidi wapatiwe mafunzo na menejimenti ya kampuni hiyo ili kufanya kazi kwa ufanisi na kuzalisha bidhaa zenye ushindani. Alisema awali walikuwa wakitegemea wafanyakazi waliosomea kutoka vyuo vya ufundi vya Mamlaka ya Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) ambavyo hata hivyo vilikuwa vikizalisha wafanyakazi wachache ambao nao hawakidhi mahitaji.
Alisema sababu kubwa ya uhaba huo wa wafanyakazi ni kutokana na aina yenyewe ya kazi zinazotakiwa kufanyika katika kiwanda hicho, ambacho wengi wa wataalamu wanaoajiriwa hukimbia baada ya muda mfupi wanapoajiriwa. Kwa sasa kiwanda hicho, kinaajiri Watanzania 1,800 kwa siku. Alisema kukabili uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi, wameanzisha programu maalumu ya mafunzo kwa vijana inayotekelezwa kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Kwa mujibu wa Massawe, kupitia mkataba wa EPZA, kampuni zote zilizopo chini ya mamlaka hiyo, zinatakiwa kuuza bidhaa zake kwa asilimia 80 nje ya nchi na asilimia 20 pekee ndani ya nchi. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014, EPZ katika kipindi cha miaka sita iliyopita ilizalisha ajira 32,000 katika viwanda 118 na mtaji uliowekezwa ulifikia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 1.3. Mwekezaji wa nje anayewekeza kupitia mamlaka hiyo, hutakiwa kuwa na mtaji wa kiasi cha Dola za Marekani 100,000 (Sh milioni 221) wakati mwekezaji wa ndani hutakiwa kuwa na mtaji wa Dola za Marekani 500,000 (Sh bil 1.05).