VIONGOZI wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo, wametoa salamu zao za sikukuu ya Krismasi kwa kusisitiza amani, umoja na mshikamano, lakini pia wakiunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania za kuujenga uchumi imara kupitia sekta ya viwanda.
Aidha, wameipongeza serikali chini ya Rais John Magufuli kwa kupambana na ufisadi, rushwa na kujenga taifa lenye maadili ya utumishi bora na kuitaka kusonga mbele katika kuipeleka Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati.

Jana na leo, wakristo kote nchini wameungana na wenzao duniani, kukumbuka siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Kumbukumbu hiyo huendana na misa, inayofanywa ya maombi maalumu ya kumbukumbu matendo mema ya Kristo. Gazeti hili lilifuatilia Misa za Krismasi zilizoendeshwa katika makanisa mbalimbali nchini ikiwemo Misa ya Kitaifa iliyoendeshwa na Kanisa Katoliki Zanzibar.
Makanisa mengine ambayo gazeti hili lilifanikiwa kufuatilia misa zao za Krismasi ni Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT) na Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG). Kutoka Zanzibar; Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Minara Miwili lililopo Mji Mkongwe Zanzibar, Augustine Shao ameitaka Serikali kuendelea na mipango yake ya kuifanya Tanzania ya viwanda vya kati kwa ajili ya kuongeza ajira kwa vijana wengi ambao kwa sasa wanazurura.
Kwa Dar es Salaam; Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewataka Watanzania kuutumia mwaka wa 2018, kufanya kazi kwa bidii usiku na mchana ili kuharakisha maendeleo. Kutoka Kilimanjaro, Mkuu wa Jimbo Katoliki Moshi mkoani Kilimanjaro, Askofu Isaac Amani alielezea kusikitishwa na wale wanaoitumia vibaya kaulimbiu iliyoasisiwa na Rais John Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Askofu wa Kanisa katoliki Jimbo la Morogoro, Telesphor Mkude aliwataka viongozi wa ngazi mbalimbali wa serikali, taasisi za umma, binafsi na wa kidini, kila mmoja wao kutimiza wajibu wake na kuwajibika kutoa huduma bora katika jamii kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa.
Katika Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Askofu Liberatus Sangu alisema Wakristo wote Afrika, wanatakiwa kuishi kwa amani na kuyakataa baadhi ya mataifa yanachochea vita kwa lengo la kupata soko la kuuza silaha zao za kivita wanazozitengeneza.
Kutoka Dodoma; Askofu wa Kanisa la International Evangelism Sinai la Ipagala, Sylvester Thadey aliwakumbusha wazazi na walezi, kutumia fedha zao kwa tahadhali na kujiwekea akiba kwa ajili ya kulipia ada na matumizi ya elimu.
Nako Njombe; Askofu Mkuu wa Kanisa la KKKT, Dayosisi ya Kusini, Isaya Mengele alitaka serikali kuwa wazi juu ya suala la mikataba ya rasilimali za nchi ikiwemo, gesi na uchimbaji wa chuma ya Liganga na makaa ya mawe ya mchuchuma. Salamu za Zanzibar Akitoa salamu zake, Askofu Shao aliitaka serikali kuendelea na mipango yake ya kuifanya Tanzania ya viwanda vya kati kwa ajili ya kuongeza ajira kwa vijana wengi, ambao kwa sasa wanazurura.
Shao alisema hayo wakati akitoa hotuba ya mkesha wa Krismasi katika Kanisa la Minara Miwili na kusema pia kuwa wazazi wameitikia wito wa kupeleka watoto wao shule kupata elimu ya juu na wengi kufaulu.
Alisema anaunga mkono mageuzi makubwa ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ambapo kuna matumaini makubwa ya kuwepo kwa ajira nyingi kwa vijana waliohitimu vyuo vikuu. Shao alisema anaunga mkono na kupongeza kitendo cha Rais Magufuli cha kutoa msamaha kwa wafungwa wapatao 8,153 katika sherehe za Uhuru wa Tanganyika, kuwa kimetoa matumaini mapya kwa watu waliokuwa wakiteseka Magerezani.
Alisema kitendo cha msamaha, lengo lake kubwa ni kuleta mabadiliko ya maadili na nidhamu katika Magereza nchini, ambapo matarajio makubwa ya Kanisa ni kwamba watu walioachiwa huru watakuwa raia wema baada ya kujifunza.
Alisema kuzaliwa kwa Kristo ni mwanzo wa mahusiano mapya na Mungu kwa kufanya kazi na kupambana na umasikini ambapo viongozi wanatakiwa kuongeza juhudi za kukuza uchumi. Aidha, aliwataka Wakristo kuendeleza kudumisha amani nchini kwa kuwatii na kuwaheshimu viongozi waliopo madarakani. Alisema bila ya amani ya kweli hakuna ustawi mzuri wa uchumi na maendeleo.
Aidha, Askofu wa Kanisa la TAG lililopo Kariakoo mjini Unguja, Donath Kaganga amewataka Watanzania kupokea mabadiliko yaliyopo sasa ambayo lengo lake ni kuleta ufanisi na uwajibikaji katika sehemu za kazi. “Mabadiliko hayawezi kuja kwa mara moja... yanahitaji muda na subira, ni sawa na mambo ambayo yalimkuta Bwana Yesu katika kipindi chake cha maisha,” alisema.
Dar es Salaam Kutoka Dar es Salaam, Watanzania wametakiwa kuutumia mwaka ujao wa 2018 kufanya kazi kwa bidii usiku na mchana ili kuendeleza amani ya nchi. Mwito huo ulitolewa na Kardinali Pengo wakati akihubiri kwenye Mkesha wa Krsimasi, uliofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Maurus lililopo Kurasini, Dar es Salaam. Kardinali Pengo alisema kufanya kazi kwa bidii ni msingi mkubwa wa amani duniani na kuwa katika kujenga na kuendeleza misingi ya amani ni lazima Watanzania wafanye kazi kwa bidii.
Alisema kwa kufanya kazi, wananchi watapata kipato kinachostahili na hata uhalifu unaweza kupungua katika jamii na hivyo amani kuendelea kuwapo. “Ninachowaomba ni kufanya kazi na tena zile zinazompendeza Mungu na kulinda utu wa watu. Kwa kufanya hivyo ni lazima jamii itabadilika na hivyo kuendana na dhana ya serikali ya kuwa na jamii ya amani zaidi,” alisema Pengo.
Alitoa mwito pia kwa Watanzania kumwombea Rais Magufuli na serikali yake ili waweze kuongoza jamii za Watanzania kwa amani zaidi kwa miaka ijayo. Katika Kanisa la Mtakatifu Albano ilifanyika Misa iliyoongozwa na Kasisi kutoka Dayosisi ya Dodoma, John Sembuyagi ambaye pia aliwabatiza watoto zaidi ya 20. Katika mahubiri yake, aliwataka Wakristo nchini kutomwacha Mungu akae kimya na badala yake wamsumbue kwa maombi kila kukicha.
Alisema kumekuwa na Wakristo ambao huacha kuomba na kumtaka Mungu awatendee mambo mbalimbali katika maisha yao na mwisho wa siku kujikuta wakimwacha Mungu kukaa kimya dhidi yao. “Yani hata kuwaleta watoto hapa kanisani tu wakacheza cheza na kukimbia hata wakilia hiyo ni hatua nzuri ya kuwaweka watoto hao karibu zaidi na Mungu na hiyo ni ishara nzuri katika Ukristo,” alisema Sembuyagi.
Salamu za Kilimanjaro Kutoka Kilimanjaro; Mhashamu Askofu Amani alielezea kusikitishwa na wale wanaoitumia vibaya kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’. Askofu Amani ambaye pia ni msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Mbulu, aliyaeleza hayo wakati akitoa salamu zake za Krismasi wakati wa Ibada iliyofanyika Katika Kanisa la Kristu Mfalme Moshi Mjini, jana. Aidha alisema pia kuna changamoto nyingine kama vile ulevi wa pombe, dawa za kulevya, biashara ya binadamu ikiwemo ya kujiuza, ambazo alisema pamoja nyingine nyingi hazina budi kufanyiwa kazi kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Alisema zinahitajika jitihada kubwa katika kuzalisha na kuhifadhi chakula, elimu ya juu ya lishe bora, kuishi kwenye mazingira safi na kujenga utamaduni wa kutunza afya binafsi.
Aidha, alisema uaminifu ndani ya jamii pia ni changamoto. Askofu Mkude Askofu Telesphor Mkude wa Morogoro, aliwataka viongozi wa serikali, taasisi za umma, binafsi na wa kidini, kila mmoja kutimiza wajibu wake na kuwajibika kwa kutoa huduma bora katika jamii kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa. Alisema hayo jana baada ya kuongoza Ibada ya Misa Takatifu ya Krismasi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Patrice mjini Morogoro.
Hiyo ilikuwa ni ibada yake kubwa ya kwanza kuongoza tangu aliporejea hivi karibuni kutoka India alikokwenda kutibiwa. Alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya Rais Magufuli kwa kuonesha kwa vitendo dhana ya uwajibikaji kwa umma kutokana na viongozi wake kila mmoja kuwajibika katika masuala mbalimbali ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Kuhusu mmomonyoko wa maadili hususani suala la mavazi yasiyo na staha, Askofu Mkude aliunga mkono kauli ya Rais Magufuli ya kukemea tabia inayoanza kujengeka ya baadhi ya vijana na watoto kuvaa mavazi yasiyo na staha mbele ya jamii.
Alisema ni wajibu wa wazazi na walezi kujitafakari na kujitazama upya juu ya namna wanavyoshughulika na malezi ya watoto wao. Uchochezi vita Askofu Sangu wa Shinyanga, alisema Wakristo wote Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla wanatakiwa kuishi kwa amani na kuyakataa baadhi ya mataifa yanayoingia kuchochea vita kwa lengo la kutaka kuuza silaha zao za kivita wanazozitengeneza. Aliyasema hayo jana katika Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma, Parokia ya Ngokolo mjini Shinyanga katika salamu zake za Krismasi.
Amewataka waumini wa dini hiyo kuilea amani aliyoiletwa na mkombozi Yesu Kristo ambaye alisema ni Emmanuel au Noeli kwa kuzaliwa kwake na kuokoa. Matumizi mabaya ya fedha Askofu Thadey wa Dodoma, amewakumbusha wazazi na walezi kutumia fedha zao kwa tahadhari na kujiwekea akiba kwa ajili ya kulipia ada na matumizi ya elimu.
Alisema; “Sina maana ya kuwalazimisha kwenye suala la bajeti ikiwemo kwenye matumizi yenu, bali mimi kama mzazi na mtumishi ni muhimu nikawakumbusha lile ambalo lipo mbele yetu ambalo pia ni muhimu kwa kila mzazi mwenye kusomesha shule,” alisema na kuonya kusherehekea sikukuu kwa kufanya matendo yanayomchukiza Mungu.
Mchungaji Evance Chande wa Kanisa la Evangelism Assemblis of God Tanzania (EAGT) Sloam Ipagala mjini Dodoma, aliwataka Watanzania kuisheherekea Sikukuu ya Krismasi kwa kuisaidia serikali katika kuhakikisha ulinzi unakuwepo badala ya kuliachia Jeshi la Polisi pekee.
Mikataba ya rasilimali Askofu Mengele ameiasa serikali kuwa wazi juu ya suala la mikataba ya rasilimali za nchi ikiwemo, gesi na uchimbaji wa chuma ya Liganga na makaa ya mawe ya Mchuchuma. Imeandikwa na Suleiman Khatib (Zanzibar), Evance Ng’ingo (Dar), Deus Ngowi (Moshi), John Nditi (Morogoro), Kareny Masasy (Shinyanga), Sifa Lubasi (Dodoma) na Salome Mwasamale (Njombe).