Mfanyabiashara mhafidhina Sebastian Pinera ameshinda uchaguzi wa urais Chile, Juan Orlando Hernandez naye akatangazwa mshindi Honduras.
Afrika Kusini chama cha ANC nacho kinamchagua kiongozi wake:
Hizi hapa ni taarifa kuu leo kimataifa:

Mrithi wa Zuma chama cha ANC kujulikana leo

Kuna ushindani mkali kati ya Nkosazana Dlamini-Zuma na Cyril RamaphosaHaki miliki ya pichaREUTERS/AFP
Image captionKuna ushindani mkali kati ya Nkosazana Dlamini-Zuma na Cyril Ramaphosa
Chama tawala nchini Afrika Kusini ANC kinapiga kura kumchagua atakayemrithi rais Jacob Zuma kama kiongozi wa chama hicho. ANC kilisema kimebadilisha uamuzi wake wa awali kuchelewesha kura hiyo hadi leo Jumatatu.
Takriban wajumbe elfu tano wanamchagua kati ya makamu wa rais Cyril Ramaphosa na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje Nkosazana Dlamini-Zuma.

Pinera ashinda urais Chile

Sebastián Piñera ataongoza kwa muhula wa piliHaki miliki ya pichaMARTIN BERNETTI
Image captionSebastián Piñera ataongoza kwa muhula wa pili
Mojawapo ya matajiri Chile, mfanyabiashara mhafidhina Sebastian Pinera, ameshinda duru ya pili ya uchaguzi wa urais jana Jumapili. Amejinyakulia karibu asilimia 50 ya kura zilizopigwa na kumshinda seneta wa mrengo wa kushoto ambaye pia ni mwandishi habari Alejandro Guillier kwa asilimia 10. Bwana Pinera ameahidi kuwapa raia wote Chile maisha mazuri zaidi.

Hernandez rais mpya wa Honduras

Juan Orlando HernándezHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionJuan Orlando Hernández ameongoza taifa hilo tangu 2013
Tume ya uchaguzi nchini Honduras imemtangaza kiongozi aliyepo Juan Orlando Hernandez, mshindi wa uchaguzi wa mwezi jana wa urais, licha ya maandamano ya wiki kadhaa kutoka upinzani wanaolalamika kuwepo udanganyifu.
Hernandez amemshinda mtangazaji mashuhuri wa televisheni, Salvador Nasralla, kwa asilimia chini ya mbili.
Upinzani umewaomba raia wamiminike barabarani kupinga uamuzi huo.

Suu Kyi alaumiwa kwa kuwakandamiza Waislamu wa Rohingya

Suu KyiHaki miliki ya pichaEPA
Mkuu wa haki za binaadamu katika Umoja wa mataifa ameiambia BBC kwamba anachukulia kuwa kiongozi wa Myanmar, Aung San Suu Kyi, ameagiza ukandamizaji wa jamii ndogo ya waislamu Rohingya.
Zeid Ra'ad Al Hussein amesisitiza kwamba maamuzi yamechukuliwa kutoka ngazi ya juu, kutokana na ukubwa wa operesheni ya kijeshi iliyosababisha kuuawa kwa maelfu ya watu.

Trump asema hajapanga kumfuta kazi Mueller

Robert Mueller ni mkuu wa zamani wa FBIHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionRobert Mueller ni mkuu wa zamani wa FBI
Rais Trump amesema hana nia ya kumfuta kazi mwendesha mashtaka maalum, Robert Mueller, anayechunguza tuhuma za Urusi kuingilia kati uchaguzi wa urais wa Marekani.
Alipoulizwa hapo jana iwapo atamtimua Mueller, aliwajibu waandishi habari, "hapana, sitomfuta."

Kadi ndogo zaidi ya Krismasi

Wanasayansi wa Uingereza wanasema wameunda kadi ndogo duniani ya Krismasi. Ni ndogo kiasi cha kuwa, kadi milioni mia mbili kama hiyo zinaweza kutosha katika stampu moja ya posta. Kadi hiyo ina picha ya sanamu la theluji juu ya ujumbe ulioandikwa "salamu za msimu", na ina ujumbe mwingine ndani ya kadi hiyo.