JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesisitiza kuwa ni marufuku kupiga fataki au kuchoma matairi Mwaka Mpya katika eneo lolote ndani ya Dar es Salaam na watakaofanya hivyo kukamatwa.
Pia, limesema litafanya doria kwa kutumia askari watakaotembea kwa miguu, farasi, mbwa na magari kuzunguka katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo wakati wa sikukuu hiyo.

Lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha hali ya amani na utulivu, inatawala katika jiji hilo kubwa la kibiashara Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alipozungumza na waandishi wa habari wiki hii kuhusu sikukuu za mwisho wa mwaka.
Mambosasa alisisitiza kuwa jeshi la polisi, halitamvumilia mwananchi yeyote, atakayepiga fataki au kuchoma matairi Mwaka Mpya katika eneo lolote ndani ya Dar es Salaam, isipokuwa wale watakaoheshimu sheria na kwenda Kawe, eneo lililotengwa maalumu kwa ajili hiyo.
“Tunawataka wananchi kuepuka kupiga fataki na kuchoma matairi katika kipindi hiki cha sikukuu, hususani Mwaka Mpya. Tunawataka wote wenye nia ya kupiga fataki kwenda katika uwanja wa kilichokuwa kiwanda cha Tanganyika Packers (Kawe) na kukidhi matakwa yao,” alisema kamanda huyo.
Mambosasa aliwataka wakazi wa mkoa huo kuwa makini wakati wote wa shamrashamra za sikukuu ya Mwaka Mpya ili kuepuka kuingia katika mikono ya sheria kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ya ulevi kwa baadhi ya madereva.
“Tunaendelea kusisitiza kuwa kila mtu asherehekee sikukuu kwa amani, hatutakuwa na simile ya aina yoyote kwa mtu yeyote atakayevunja sheria kwa makusudi ili mradi ajifurahishe nafsi yake na kuleta karaha au kuhatarisha usalama kwa wengine,” alisema Mambosasa.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi liliwatangazia wananchi hivi karibuni kuwa ukiona wahalifu au uhalifu unatendeka katika maeneo yao au mahali walipo, tafadhali wapige simu namba 111, 112 na 0787 668306