Kiongozi wa zamani wa Gambia Yahya Jammeh ambaye aliondoka madarakani na kuihama nchi hiyo mwaka uliopita baada ya kutawala kwa miongo miwili ametuhumiwa kutenda makosa mengi.
Lakini moja ya makosa hayo ni jambo la kushangaza - kuwalazimu maelfu ya watu waliokuwa na virusi vinavyosababisha Ukimwi kunywa dawa yuke ambayo alidai kuivumbua.
Dawa hiyo ilikuwa mchanganyiko wa mitishamba.
Mwandishi wetu Colin Freeman anasema watu kadha walitafiki baada ya kutumia tiba hiyo kutoka kwa Bw Jammeh.
Lamin Ceesay, mtu wa kwanza kutangaza hadharani kwamba alikuwa na virusi vya Ukimwi nchini Gambia, alifikiria kwamba alikuwa anafanya jambo la busara sana.
Ilikuwa mwaka wa 2000, na ufahamu kuhusu Ukimwi Afrika bado haukuwa pevu, na waliokuwa na virusi hivyo walikabiliwa na unyanyapaa na kubaguliwa sana katika jamii.
Siku ya Ukimwi Duniani mwaka huo, Ceesay alijipatia ujasiri na kutangaza hadharani kwamba alikuwa na Virusi Vinavyosababisha Ukimwi (VVU).
Alishiriki pia matembezi ya kuhamaisha watu kuhusu virusi hivyo, ambayo yaliandaliwa na shirika moja la hisani.
Hatua hiyo ilimpa umaarufu na kumfanya kuheshimiwa na wahamasishaji wa jamii kuhusu Ukimwi duniani.
Lakini miaka michache baadaye, aliangaziwa na Rais wa Gambia Yahya Jammeh.
Ilikuwa ni mapema mwaka 2007, Jammeh alipotangaza kwamba alikuwa amevumbua tiba ya ajabu ya virusi hivyo, ilikuwa ni mchanganyiko wa dawa za mitishamba na mbinu nyingine za kiroho za kuwatibu wagonjwa.
Jambo lililoshangaza hata zaidi ni kwamba Jammeh alisema tiba hiyo ilifanya kazi Alhamisi na Jumatatu pekee.
Si ajabu kwamba hatua ya Jammeh ilishutumiwa vikali na wakuu wa afya duniani.
Lakini nchini Gambia kwenyewe, kumwambia rais kwamba alikuwa anahubiri upuzi lilikuwa jambo ambalo hungethubutu, ungejipata jela.
Kwa hivyo, shirika la Ukimwi alilokuwa anafanyia kazi Ceesay lilipopokea barua, ikiomba watu 10 wajitolee kwenda kufanyia majaribio dawa hiyo ya rais kwa miezi sita, aliamua hangeachwa nyuma.
Alijitolea.
"Nilifikiria kwamba kuhusu kuwatuma watu wengine tu kwa mpango huo, lakini nilihofia kwamba iwapo zingeenda nami pia, ningekuwa matatani," aliniambia.
"Nilifikiria, 'Mbona nisiende? Haiwezi kunidhuru'."
Lakini Ceesay alikuwa amenoa.
Ilikuwa ni hadi alipofika katika kliniki ya muda ya rais katika ikulu ambapo walifafanuliwa sheria za mpango huo.
Hakuna uvutaji sigara, au kunywa chai au kahawa.
Hakuna kushiriki ngono.
Na muhimu zaidi, hakuna kunywa dawa za kuundiwa viwandani - ikiwa ni pamoja na dawa za kupunguza makali ya Ukimwi ambazo zilikuwa zinatolewa na madaktari.
Hangerudi nyuma tena, hata hivyo.
Walinzi wa Jammeh wakiwa na silaha walikuwa wanalinda lango la kliniki hiyo usiku na mchana.
Kwa miezi sita iliyofuata, walisema, hakuna mgonjwa ambaye angeruhusiwa kuondoka bila idhini ya Jammeh.
Na hapo basi, tiba ikaanza.
Kila siku asubuhi, rais angefika na kuwapaka dawa iliyofanana na mafuta mwilini, huku akisema sala kutoka kwa Koran ambayo ilikuwa na jalada la ngozi.
Kisha, mara mbili kwa siku, walilazimishwa kunywa mchanganyiko wa mitishamba wa rangi ya manjano kutoka kwenye chupa.
Jammeh alikataa kusema dawa hiyo ilikuwa na nini, licha yake kuambiwa kwamba iwapo Jammeh alikuwa amevumbua tiba ya Ukimwi basi Gambia ingekuwa tajiri ghafla.
Dawa hiyo ilimfanya Ceesay kuhara sana.
Aidha, aliambukiwa kifuakikuu na wagonjwa wengine, na mwishowe akadhoofika kiafya kiasi kwamba ililazimu kurejeshwa hospitali ya kawaida.
Baada ya kupimwa, ilibainika kwamba kiwango chake cha virusi mwilini kilikuwa kimepanda sana, na akaanza kupewa dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo tena.
Ceesay alikuwa miongoni mwa waliokuwa na bahati.
Mkewe, ambaye alikuwa anaugua Ukimwi pia, alifariki akipokea tiba hiyo ya rais, sawa na wagonjwa wengine wengi waliokuwa pamoja naye.
"Kama mtu mashuhuri miongoni mwa waliokuwa na Ukimwi, nilikuwa nahudhuria mazishi kila wakati," anasema.
Hali hiyo, hata hivyo, ilikuwa tofauti sana na aliyojaribu kuionesha Rais Jammeh ambaye aliwalazimisha wagonjwa kutokea kwenye televisheni kusifu ufanisi wa mpango huo.
Miongoni mwao alikuwa Ousman Sowe, aliyekuwa na shahada ya kwanza katika afya ya umma kutoka kwa chuo kikuu cha Leeds, Uingereza.
Jammeh, katika juhudi za kuupa mpango wako usomi kiasi, alikuwa amemwita Sowe na kumteua kuwa msemaji wake, kujaribu kuwapuuzilia mbali wanahabari wa kigeni waliokuwa na maswali chungu nzima.
Wakati mmoja, Sowe aliambia mwanahabari wa BBC kwamba alikuwa na "imani 100%" kuhusu tiba hiyo.
Ukweli ni kwamba, kutotumia dawa za kupunguza makali ya VVU kulimfanya kudhoofika kiasi kwamba hangeweza kupanda ngazi kwenye majumba.
"Kama mtu aliyekuwa amesoma, nilijua ulikuwa upuuzi," anakumbuka Sowe.
"Lakini singesema chochote dhidi ya mpango huo, ingawa watu walikuwa wanafariki dunia."
Sowe na wagonjwa wenzake walionusurika sasa wanafanya kazi na shirika la Aids-Free World kutoka Marekani ambalo linataka Jammeh ashtakiwe kutokana na mpango huo.
Shirika hilo linasema huo ndio pengine moja ya ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu ambao ulitekelezwa na utawala wa Jammeh.
La kusikitisha zaidi ni kwamba tofauti na magereza ya kisiri na vyumba vya mateso, ni mpango ambao uliendeshwa ulimwengu wote ukitazama.
Jammeh hakuwa na wasiwasi kuhusu hilo hata hivyo.
Afisa wa ngazi ya juu ya Umoja wa Mataifa aliyeupinga mpango huo alifukuzwa nchini Gambia.
Inaaminika kwamba jumla ya watu 9,000 walipokea tiba hiyo.
Kwa kuwa Jammeh aliweka siri nyaraka za mpango huo, hakuna mtu yeyote ambaye amebaini idadi kamili ya waliofariki.
Jambo moja ni wazi hata hivyo - kwamba mwujiza pekee kuhusu tiba hiyo ni kwamba kuna watu walinusurika.
Picha na Colin Freeman
|
0 Comments