POLISI nchini Guinea imesema inamshikilia mganga wa kienyeji anayetuhumiwa kuwalaghai mamia ya wanawake, kuwa watapata mimba. Mganga huyo, N’na Fanta Camara aliwapatia wanawake hao ambao hawakuwa na uwezo wa kupata ujauzito majani mchanganyiko na mimea mbalimbali, iliyosababisha matumbo ya wanawake hao kufutuka na kuonekana kama wana mimba.

Kutokana na huduma yake hiyo, wateja wa mganga huyo walilipa dola za Marekani 33. Pato la wastani la mwananchi wa nchi hiyo ni dola za Marekani 48. Jeshi la Polisi linasema Camara alishawishi mamia ya wanawake hao kumlipa kiasi hicho cha dola za Marekani kwa mwezi.
Lakini, mwenyewe anadai kuwa alikuwa anajaribu kuwasaidia. Zaidi ya wanawake 700 wenye umri kati ya miaka 17 hadi 45, wameathirika na dawa hiyo ya kuwafanya wawe na mimba, badala ya kuwatibu matatizo yao ya uzazi.
Idadi hiyo kubwa inaonesha ni jinsi gani Guinea na nchi nyingine za Afrika, zinavyotegemea zaidi kwa waganga wa kienyeji kutatua masuala mbalimbali, ikiwemo ya uzazi. Mwaka 2006 Shirika la Afya Duniani (WHO), lilibainisha kuwa asilimia 80 ya Waafrika wanatumia tiba za kienyeji. Kwa mujibu wa daktari kutoka jeshi la polisi, wanawake walitumia dawa hizo wakakabiliwa na matatizo ya kiafya kwa muda mrefu.
Mmoja wa wanawake hao aliyepata tiba ya uzazi kwa Camara, Alhassan Sillah alisema amekuwa akitumia tiba za mganga huyo wa kienyeji kwa kipindi cha mwaka mmoja. “Siku yangu ya kwanza nilipoenda alinipatia majani na mimea mingine ambayo baada ya kuinywa nilitapika. Alinihakikishia kuwa hiyo ni dawa bora itakayomaliza tatizo langu la kukosa mtoto. Kadri nilivyoendelea kunywa dawa hizi, tumbo langu lilianza kujaa,” alisema Sillah.
Alisema baada ya kuona dalili hiyo njema, alienda tena kwa mganga huyo ambaye baada ya uchunguzi wake, alidai kuwa tayari amefanikuwa kupata mimba. Hata hivyo, kwa mujibu wa Sillah, mganga huyo aliwaonya wanawake hao wote kutokwenda kwa madaktari wa kawaida. “Baada ya kutuambia tuna mimba, tulitakiwa kumpatia kuku na nguo,” alisema. Alibainisha kuwa hakuna hata mwanamke mmoja, aliyefanikiwa kujifungua mtoto, zaidi ya kuonekana kama wana mimba kwa kipindi cha miezi 12 hadi 16.