Mshambuliaji wa klabu ya Girona nchini Uhispania, Mkenya Michael Olunga ameweka historia siku ya Jumamosi , na kuwa mchezaji wa kwanza wa Kenya kufunga hatrick katika ligi ya Uhispania huku wakiishinda klabu ya Las Palmas 6-0.

Olunga aliingia kama mchezaji wa ziada na kufunga katika dakika ya 57, 70 na 79 na kuwa mshambuliaji wa kwanza wa klabu ya Girona kufunga hat-rick katika msimu wake wa kwanza katika ligi ya La Liga.
Ushindi huo ulikuwa mkubwa kwa klabu hiyo ya Catalan tangu iingie katika ligi ya La Liga.
Olunga mwenye umri wa miaka 23 anaichezea Girona kwa mkopo kutoka klabu ya China ya Guizhou Hengfeng.
Girona walikuwa mbele baada ya kipindi cha kwanza kupitia bao la penalti .
Mchezaji huyo wa Kenya alifunga krosi murua iliopigwa na Johan Mojica na kuongeza uongozi wa Girona kabla ya kuchangia katika bao lilofungwa na kiungo wa kati wa klabu hiyo Borja Garcia.
Makosa ya walinzi wa Las Palmas yalimfanya Olunga kuongeza bao la nne kabla ya kumpatia pasi nzuri Cristian Portu aliyefunga bao la 5.
Baadaye Olunga alifunga bao la sita na hat-rick yake ya kwanza kwa urahisi dakika 11 kabla ya kukamilika kwa mechi hiyo.